1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waliokufa kwa tetemeko Japan wafikia 62

3 Januari 2024

Idadi ya vifo kutokana na tetemeko kubwa la ardhi lililoikumba Japan katika Siku ya Mwaka Mpya imeongezeka na kufikia watu 62 huku mamlaka ikiwa katika jitihada ya kuwasaidia manusura nchini humo.

Japan Erdbeben Wajima
Kikosi cha zimamoto kikiwa katika juhudi za kunusuru watu katika jengo lililoporomoka mjini WajimaPicha: Kyodo News/AP Photo/picture alliance

Jumatatu alasir tetemeko hilo lenye ukubwa wa kipimo cha 7.6 lilipiga eno la Noto, kuzisambaratisha nyumba na kusababisha ugumu wa kufikisha misaada ya kiutu yenye kuhitajika sana katika maeneo ya mbali ya taifa hilo.

Mvua kubwa imetabiriwa katika maeneo yaliyokumbwa na tetemeko hilo Jumatano hii na hivyo kuongeza hofu ya maporomoko ya ardhi. Taarifa hiyo imezusha hofu kwa juhudi za serikali katika kuwanusuru watu wengi ambao wamenasa kwenye vifusi.

Athari za tetemeko bado kitendawili hadi sasa

Barabara zimeharibika vibaya, miundombinu imebomoka, na maeneo ya mbali ambayo yameathirika vibaya imekuwa vigumu kufikika na kufanikisha juhudi za uokozi. Hadi wakati huu taarifa kamili za athari zilizotokea bado hazijaweza kufahamika ikiwa ni takribani siku mbili baada ya kutokea balaa hilo.

Eneo la soko lililoungua katika mji wa WajimaPicha: The Yomiuri Shimbun via AP Images/picture alliance

Kwa mfano huko Suzu, mji wenye zaidi ya kaya 5,000 ulio karibu na kitovu cha tetemeko, mamlaka zimeshindwa kujibu miito takriban 72 ya msaada, kwa mujibu wa meya wake Masuhiro Izumiya. Hadi wakati huu mamlaka ilithibitisha vifo 62, kutoka idadi ya awali ya watu 55 ambayo ilitangazwa Jumanne, takwimu ambazo zinalifanya tetemeko hilo kuingia katika rekodi mbaya zaidi tangu 2016.

Kauli ya Waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari Waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida alisema "Imekuwa zaidi ya saa 40 tangu tetemeko la kwanza kutokea. Hii ni vita dhidi ya wakati, na ninaamini sasa ni wakati muhimu sana wa vita hivyo." Alikuwa akitoa taarifa baada kikao cha kukabiliana na maafa nchini humo.

Askari wa zimamoto wakiwa katika jitihada ya kusaka watu katika mji wa WajimaPicha: The Yomiuri Shimbun via AP Images/picture alliance

Serikali imefungua njia ya bahari kupeleka misaada na baadhi malori makubwa sasa yanaweza kufikia katika baadhi ya maeneo yaliyoathirika zaidi.

Mitsuru Kida mwenye umri wa miaka 74, manusura wa tetemeko la ardhi anayeishi Jiji la Wajima lenye hali ngumu, anaonesha hofu ya kwamba kurejea kwa maisha ya kawaida katika maeneo yake  utakuwa mchakato wa muda mrefu.

Soma zaidi:Tsunami yaipiga Japan

Mwaka 2011, nchi hiyo kwa upande wa kaskazini/mashariki ilikumbwa na tetemeko kubwa la ardhi la ukubwa wa 9.0 katika kipimo cha Richter,  ambalo lilisababisha tsunami iliyosababisha vifo vya takriban watu 18,500.

Chanzo: RTR

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW