1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya maambukizi ya corona yashuka Uhispania

Daniel Gakuba
30 Machi 2020

Uhispania imesema inashuhudia ishara za kupungua kwa kasi ya maambukizi ya virusi vya corona, licha kuripotiwa vifo vipya zaidi ya 800 katika muda wa saa 24 zilizopita.

Spanien | Coronavirus | Madrid
Picha: Reuters/S. Perez

Na huko Israel waziri mkuu Benjamin Netanyahu amejiweka karantini, baada ya msaidizi wake kuthibitika kuwa na maambukizi ya COVID-19. 

Idadi ya watu waliokufa kutokana na virusi vya corona nchini Uhispania imepanda na kufika watu 7,340, kufuatia kutangazwa kwa vifo vipya 812 hii leo. Kwa idadi hiyo nchi hiyo ni ya pili duniani kwa kupoteza watu wengi kwa ugonjwa wa COVID-19, baada ya Italia ambako hadi sasa ugonjwa huo utokanao na virusi vya corona umeuwa watu wapatao 10,780.

Lakini licha ya idadi hiyo kubwa ya vifo, Maria Jose Sierra ambaye ni daktari kutoka kituo cha uratibu wa huduma za dharura katika wizara ya  afya nchini Uhispania, amesema wanashuhudia ishara njema za kupungua angalau kidogo, kwa kasi ya maambukizi na vifo.

Mwandishi wa habari wa Uhispania akiwa amejilinda dhidi ya virusi vya coronaPicha: picture-alliance/AA/B. Akbulut

Kuanzia Machi 25 tumeona mabadiliko katika ongezeko la visa vya maambukizi. Tangu siku tulipoanzisha mpango wa kuwataka watu kuacha kusogeleana, nchini kote Uhispania kati ya tarehe 15 hadi 25 Machi, ongezeko la visa vipya vya maambukizi vimeshuka kutoka asilimia 20 hadi asilimia 12.

Uhispania sasa imejiunga na Italia na Marekani kama nchi tatu zinazoongoza kwa wagonjwa wengi wa virusi vya corona, zikiipita China vilikoanzia virusi hivyo.

Huko nchini Israel, waziri mkuu wa nchi hiyo Benjamin Netanyahu amejiweka chini ya karantini, baada ya vipimo kuthibitisha kwamba msaidizi wake anayo COVID-19.

Tangazo la ofisi ya Netanyahu limesisitiza kuwa kujizuia nyumbani huko ni hatua ya tahadhari tu, kwa kwa muda wa angalau wiki mbili waziri mkuu huyo hajasogeleana kwa karibu na wafanyakazi wake, akiwemo mshauri huyo aliyeugua.

Rais Vladimir Putin amesema nchi yake imepiga hatua kuzuia kusambaa kwa virusi vya coronaPicha: picture-alliance/dpa/AP/Kremlin/A. Druzhinin

Kwingineko, rais wa Urusi Vladimir Putin amesema nchi yake imepiga hatua katika kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona. Akizungumza na wajumbe wake mikoani, Putin ametahadhalisha hata hivyo, kuwa hali hiyo inaweza kubadilika wakati wowote, na kutaka iwepo mipango ya kukabiliana na ongezeko la haraka.

Kwa wakati huu Urusi ni miongoni mwa nchi zenye visa vichache vya maambukizi ya virusi vya corona, kwa idadi ya wagonjwa 1,836 tu.

Na huko Afrika, hali ya taharuki imejiri katika jiji kuu la kibiashara nchini Nigeria, Lagos, baada ya rais Muhamadu Buhari kutangaza kufungwa kwa shughuli zote kwa muda wa siku 14. Umati wa watu na msongamano wa magari vimelighubika jiji hilo wakati kila mmoja alipokuwa akijaribu kununua mahitaji ya lazima kabla ya kuanza kutekelezwa kwa amri ya rais.

Mashirika:afpe, ape

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW