1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya maambukizi ya VVU yaongezeka Ulaya

1 Desemba 2022

Shirika la Afya Duniani, WHO pamoja na ofisi ya shirika hilo katika Umoja wa Ulaya yamesema kuwa watu zaidi na zaidi barani Ulaya wanaishi na virusi vya UKIMWI, bila ya kupimwa wala kugundulika.

AIDS-Aufklärungskampagnen zum Welt-AIDS-Tag
Picha: Saikat Paul/Pacific Press/picture alliance

Hayo yameelezwa Alhamisi wakati ambapo dunia ikiadhimisha Siku ya kupambana na UKIMWI Duniani kila Desemba Mosi. Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na shirika hilo, hali hiyo inaonesha kuwa bado kuna unyanyapaa dhidi ya watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI, VVU na kwamba suala hilo linapaswa kukemewa.

Ofisi ya WHO barani Ulaya imeeleza kuwa kulingana na takwimu mpya, tangu mwaka 2018 na hadi 2021, watu zaidi wameambukizwa VVU barani Ulaya kuliko wale waliokuwa wamepimwa na kugundulika kuwa na virusi hivyo.

Ofisi ya WHO katika bara la Ulaya inazihusisha zaidi ya nchi 50, ikiwemo Urusi, Ukraine na Uturuki. Kwa kulinganisha, katika eneo la Kiuchumi la Ulaya, EEA linalozijumuisha Iceland, Liechtenstein na Norway, mbali na nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, uchunguzi zaidi wa VVU kuliko maambukizi uliripotiwa katika muongo mmoja uliopita. Hali hiyo inaonesha kuwa idadi ya watu ambao hawajapimwa kwenye nchi hizo ilikuwa ikishuka.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO barani Ulaya, Hans KlugePicha: HANS PUNZ/APA/picturedesk.com/picture alliance

Mkurugenzi Mkuu wa WHO barani Ulaya, Hans Kluge amesema wanapaswa kuwa na wasiwasi mkubwa kutokana na takwimu za upimaji wa VVU, matibabu na huduma. Kluge anasema kuendelea kuenea kwa unyanyapaa dhidi ya VVU kunawazuia watu kupima na kunawafanya wasifikie lengo lao la mwaka 2030 la kuumaliza kabisa ugonjwa wa UKIMWI.

WHO pia imetaka huduma za VVU ziweze kupatikana zaidi na washirikiane ili kuhakikisha kwamba hakuna mtu anayehisi anaogopa wala kuona aibu kupimwa, au kukata tamaa au kutengwa kutokana na hali yake. Kluge amesema kila mmoja, popote pale anapaswa kupata huduma na matunzo ya heshima anayohitaji.

Kupima VVU ni muhimu

Aidha, Mkurugenzi wa Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Ulaya, ECDC, Andrea Ammon amesisitiza umuhimu wa kupima VVU, akisema wale wanaochelewa kugundulika, wana uwezekano mkubwa wa kuumwa sana na hata kufariki.

Ammon amezungumzia pia hatari ya afya ya umma, akisema watu walioathirika na VVU wasipotibiwa wanaweza kuwaambukiza wenza wao VVU bila kujua.

Kwa mjibu wa WHO, mwaka 2021, takribani watu 300 waligundulika kuwa na VVU kila siku katika nchi 46 kati ya 53 za Ulaya, pamoja na visa 45 kila siku katika nchi za EEA.

Mkurugenzi Mkuu wa UNAIDS, Winnie ByanyimaPicha: Ryan Remiorz/Zuma/IMAGO

Wakati huo huo, katika ujumbe wake wa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani kwa mwaka 2022, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la UKIWMI, UNAIDS, Winnie Byanyima amesema katika eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, wasichana na wanawake wana uwezekano mkubwa wa kuambukizwa VVU mara tatu zaidi ya wavulana na wanaume wa rika moja.

Anasema sababu kubwa ni kukosekana kwa usawa. Byanyima amebainisha kuwa kuwaruhusu washichana kumaliza elimu ya sekondari kunapunguza uwezekano wa kuambukizwa VVU kwa hadi asilimia 50.

Anasema iwapo wanajumuisha elimu ya kina kuhusu kujamiiana na hatua nyingine za kuwawezesha wasichana, basi hatari ya wao kupata maambukizi inapungua hata zaidi.

 

(DPA, UNAIDS https://bit.ly/3is1pkW)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW