Idadi ya mamilionea yaongezeka mara tatu duniani
18 Juni 2020Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la Boston Consulting Group (BCG) iliyotolewa Alhamisi ni kwamba hivi sasa idadi ya mamilionea imeongezeka mara tatu ikilinganishwa na miaka ishirini iliyopita. Nchini Ujerumani idadi ya mamilionea wake imeongezeka mara mbili.
Zaidi ya watu milioni 24 duniani wanamiliki utajiri wa dola milioni moja (sawa na Euro 891,000) au zaidi, hii ni kulingana na ripoti ya kila mwaka ya ''Global Wealth'' ya shirika la BCG kwenye toleo lake la 20, ukilinganisha na watu milioni 8.9 mwaka 1999.
Utafiti wa shirika hilo ulijikita kwenye sekta binafsi ya kifedha kuhusu wamiliki wa akaunti za benki zenye fedha. Mnamo kipindi cha miaka 20 iliyopita, utajiri wa watu binafsi uliongezeka pia mara tatu kutoka dola trilioni 80 hadi dola trilioni 226 mwishoni mwa mwaka 2019. Kwa pamoja mamilionea wote walijumuisha asilimia 50 ya jumla ya utajiri ulimwenguni, inaelezea ripoti hiyo.
Ikiwa na mamilionea 400.000, Ujerumani yenye uchumi mkubwa barani Ulaya, imeshika nafasi ya saba duniani kwa idadi ya mamilionea mwaka 2019. Idadi ya matajiri nchini ujerumani iliongezeka mara mbili mnamo kipindi cha miaka 20 iliyopita. Ujerumani inashika nafasi ya tatu duniani baada ya Marekani na China ambako idadi ya watu wanaomiliki utajiri binafsi unaozidi au sawa na dola milioni mia moja.
Mwaka jana watu 2,400 nchini Ujerumani waliorodheshwa kwenye jamii hiyo. Mabara yote yalishuhudia ongezeko la matajiri mnamo kipindi cha miaka 20 iliyopita, inaelezea ripoti ya BCG.
''Mnamo miaka 20 iliyopita hatujawahi kushuhudia kukuwa kwa aina moja baina ya maeneo kama mwaka huu wa 2019'', alisema msimamizi wa ripoti hiyo Anna Zakrzewski. Pato la matajiri binafsi kwenye nchi zinazoendelea, Asia, Mashariki ya Kati, Afrika, Amerika Kusini na Ulaya Mashariki iliongezeka kutoka moja juu ya kumi na kufikia robo ya jumla ya utajiri duniani mnamo kipindi cha miaka 20 iliyopita.
China pekee idadi ya matajiri wake wanaomiliki zaidi ya dola milioni 100 iliongezeka mara 29 mnamo kipindi cha miaka 20 iliyopita.