1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya ndovu Kenya yafikia 36,280: KWS wahamisha ndovu 50

15 Oktoba 2024

Idadi ya ndovu nchini Kenya imeongezeka zaidi ya maradufu na kufikia 36,280. Hali hii imeilaazimu idara ya wanyamapori (KWS) kuwahamisha tembo 50 kutoka hifadhi ya kitaifa ya Mwea hadi Aberdares ili kupunguza msongamano.

Kenya | Ndovu akisubiri kuhamishwa
Ndovu akisubiri kuhamishwaPicha: Thelma Mwadzaya

Helikopta na Sindano za Usingizi

Shughuli hiyo ya kuwachoma sindano ya usingizi ndovu huanza asubuhi kabla ya wanyama kuchoka na jua kupanda. Wakiwa kwenye ndege aina ya helikopta, wataalam wa idara ya wanyamapori walianza kwa kuwachoma mshale wa dawa ya usingizi ndovu hao. Pindi dawa inapoanza kufanya kazi, ndovu anadondoka kwa usingizi na ndipo kazi ya kumnyanyua inaanza.

Hifadhi ya kitaifa ya Mwea kwa sasa ina ndovu 156, idadi iliyoongezeka kutoka 49 katika miaka ya sabini. Je, hatua zipi zilizochukuliwa za uhifadhi zilizoiongeza idadi ya tembo? Rebecca Miano ni waziri wa utalii na wanyamapori nchini Kenya na anakiri kuwa, “kupitia KWS, wakaazi wa huko Mwea sasa wamepata elimu ya ulinzi wa ndovu ili waongezeke. Hapo Mwea ni mahali pazuri kwa ndovu kuzaana... kuwinda na ujangili umepungua,” anafafanua.

Wataalam wa wanyama wa KWS wakihakikisha ndovu yuko salama kabla kuhamishwaPicha: Thelma Mwadzaya

Sensa ya Wanyamapori

Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2021 ya wanyamapori, idadi kamili ya ndovu nchini Kenya imefikia 36,280. Kilichochangia ni sheria mpya iliyozindua mpango wa kitaifa wa tembo wa 2023 hadi 2032 kwa ushirikiano kati ya idara ya wanyamapori KWS na washirika wake. Dhamira ni kuwalinda ndovu waliopo, kupunguza mivutano kati ya wanyamapori na binadamu, kufufua mazingira yaliyoharibika na kuzinufaisha jamii zinazoishi kwenye maeneo yaliyo na wanyama hao.

Soma pia: Ukame waua tembo 205 nchini Kenya

Itakumbukwa kuwa katika miaka ya kati ya 1979 na 1989, idadi ya ndovu ilipungua kutoka laki 170 hadi alfu 16. Uzinduzi wa idara ya wanyamapori ya Kenya, KWS, kupitia sheria ya bunge ndiyo uliochangia kwa kiasi kikubwa kuiongeza idadi kamili ya ndovu.

Uhamishaji wa Ndovu

Azma ya idara ya wanyamapori, KWS, ni kuwahamisha ndovu 50 kutoka hifadhi ya kitaifa ya Mwea hadi ile ya Aberdares. Shughuli hiyo ilianza mwanzoni mwa Oktoba. Je, wakaazi wa maeneo yanayopakana na hifadhi ya Mwea wana mtazamo upi? Mchungaji Sili Makau ni mkaazi wa Makima iliyo nje ya hifadhi ya wanyamapori ya Mwea na anasema “sisi tunaona ni vizuri sana kuwahamisha hao ndovu kwa sababu walikuwa wameongezeka na idadi yao iliwafanya watoke nje ya hifadhi na kuingia mashambani mwa wakaazi. Hata hivyo ni mali yetu na tunaifurahia, kwa hivyo muhimu kulinda maslahi yao,” anaelezea.

Ndovu akiandaliwa kuingizwa tunduni kwenye kasha litakalomsafirishaPicha: Thelma Mwadzaya

Shughuli ya kuwahamisha ndovu 50 imeigharimu serikali shilingi milioni 12 na ilianza mwanzoni mwa mwezi huu wa Oktoba. Zoezi hilo linashabihiana na mkakati mpya wa 2024-2028 wa KWS uliozinduliwa hivi karibuni, ulio na azma ya kuwalinda ndovu, kuhifadhi mazingira, kuzishirikisha jamii zinazooishi pembeni ya mbuga na hifadhi za wanyamapori kwa manufaa ya wote.

Soma pia: Kenya yateketeza marundo ya pembe za tembo

Helen Wanja ni mkaazi wa Namuri na anaamini kuwa majirani zao wa kaunti ya Nyeri pia wana haki ya kuwaona ndovu kila wakati kwani, “Ikiwa hao hawana wanyama hawa huko, ni sawa nao pia wapelekewe wengine ili wafurahie. Kukinyesha sana ndovu hutoroka na kuingia mashambani kwa vile ni wengi, kwa hivyo ni sawa wakienda huko,” anamalizia.

Teknolojia ya Ukanda wa Shingo

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Wanyamapori wa KWS, Erastus Kanga, ili kuwafuatilia ndovu hao waliohamishwa, wataalam huwavalisha ukanda maalum wa shingo wa kidijitali na, “Tulimvalisha ndovu wa kike ambaye ndiye mama ukanda wa shingoni wa dijitali. Hilo litatuwezesha kumfuatilia yeye na familia yake... tutaweza kujua waliko kila wakati ili tuelewe wanachokifanya. Mbinu hii itaimarisha ulinzi wao kila wakati,” anafafanua.

Wataalam wa KWS wakifunga kasha la kumsafirishia ndovuPicha: Thelma Mwadzaya

Uhamishaji wa ndovu ni kiungo muhimu katika uhifadhi wa mazingira na mfumo mzima wa ikolojia. Hifadhi ya wanyamapori ya kitaifa ya Mwea ina uwezo wa kukimu ndovu kiasi ya 50, ila kwa sasa idadi humo imefikia 156. Kwa upande wa pili, hifadhi ya Aberdares iliyoko kaunti ya Nyeri ni kubwa zaidi na imezungushiwa uzio wa umeme kote ili kuwazuwia ndovu waliopotea njia na kuwalinda wakaazi wa maeneo ya karibu. Ikumbukwe kwamba sensa ya kitaifa ya wanyamapori iliyoanza katikati ya mwaka huu itahitimishwa 2025.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW