Idadi ya ndovu na faru yaongezeka tena Tanzania
10 Julai 2019Ofisi ya rais wa Tanzania imesema idadi ya ndovu na faru imeanza kuongezeka tena baada ya serikali kuivunja mitandao ya uhalifu wa kupanga, iliyokuwa inaendeshai ujangili wa kiwango kikubwa. Mfanyabiashara maarufu wa Kichina aliepewa jina la utani la "Malkia wa pembe za ndovu" alihukumiwa kifungo cha miaka 15 gerezani na mahakama nchini Tanzania mwezi Februari, kwa makosa ya usafirishaji kimagendo zaidi ya pembe 350 za ndovu barani Asia, katika ushindi mkubwa kwa serikali. Taairfa kutoka ofisi ya rais imesema katika matokeo ya kikosi kazi maalumu kilichoundwa mwaka 2016 kupambana dhidi ya ujangili, idadi ya ndovu imeongezeka kutoka 43,330 mwaka 2014 hadi zaidi ya 60,000 hivi sasa. Idadi ya faru, ambao ni spishi iliyoko katika hatari ya kutoweka, imeongezeka kutoka wanyama 15 tu hadi 167 katika kipindi cha miaka minne, imeongeza taarifa hiyo.