1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya Tembo yaongezeka nchini Kenya

20 Mei 2026

Juhudi za kuhifadhi wanyamapori zimepata msukumo mpya baada ya takwimu mpya kuashiria kuwa idadi ya tembo nchini Kenya imeongezeka kwa alfu tano na kufikia tembo 42,100.

Afrika zwei Elefanten, die einen anderen Elefanten am Schwanz halten
Picha: Tommy Mees/Pond5 Images/IMAGO Images

Idadi ya ndovu imeongezeka kutokea alfu 36,300 mwaka 2021 hadi alfu 42,100 kulingana na takwimu mpya za tathmini ya uchumi ya mwaka 2026. Ongezeko hilo ni ishara ya mafanikio ya kupambana na ujangili moja kwa moja.

Tembo wengi zaidi wanapatikana kwenye mbuga za maeneo ya Mara,  Tsavo, Amboseli na Laikipia-Samburu. Regina Metiaki ni mkaazi wa Ilmotiok huko kaunti ya Laikipia na anakiri kuwa ndovu wamerejea kwa wingi maeneo ya mbugani wanakoishi.

"Hatutaki hata ndovu wapigiwe kelele...maana hapo ndio tunapata chakula na hela za kusomeshea watoto wetu. Kuna wakati ndovu walitoweka lakini kwa sasa wako wamerejea. Watu wapende ndovu maana ni mnyama mzuri aliye na faida.Watalii wanakuja kuwatazama ndovu...hilo linatuletea fedha za kigeni….hata sisi kina mama wa Kimaasai tunawapenda ndovu maana ndio wanaotupa pato letu kutuwezesha kulea watoto.”

Thuluthi mbili ya idadi ya ndovu wote nchiniKenya wanaishi nje ya mbuga rasmi na hifadhi za wanyamapori na wanatangamana na binadamu ambao ni wakaazi wa sehemu hizo. Kadri idadi ya ndovu inavyoongezeka ndivyo migogoro kati ya binadamu na wanyamapori inavyoongezeka.

Hali hiyo imelifanya shirika la wanyamapori nchini Kenya, KWS, kutumia mbinu kama kuwahamisha wanyama hao kutokea hifadhi moja hadi nyengine ili kupunguza msongamano. Mwishoni mwa mwaka 2024,KWS iliwahamisha ndovu 50 kutokea Hifadhi ya taifa ya Mwea hadi mbuga ya Aberdares.

Mpango wa taifa wa kuhifadhi ndovu wa mwaka 2023 hadi 2032 unajikita katika kulinda mazingira wanayoishi pamoja na kuzuwia migogoro kati ya tembo na binadamu ili idadi istawi. Jim Justus Nyamu ni mwanaharakati na mtetezi wa Ndovu na anaamini mafanikio hayo yanaweza kuimarishwa japo changamoto zipo.

"Kwenye wale tembo walikuwa, maeneo yake ya lishe yanapungua kwani binadamu wanayanyemelea. Ni kweli tembo wanaongezeka lakini sio wanyama wote wanaoongezeka. Mfano fisi, idadi yake imepungua...chanzo cha hilo ni kuwa fisi anakula mabaki yanayoachwa na kunguru na simba. Simba nao pia idadi yao imepungua. Kama kule Nakuru idadi ya nyati imeongezeka lakini simba walioko pale hawawezi kuwaua nyati kwani ni wakubwa. Inabidi sasa wawinde swara kisha idadi yao inapungua.Ndiposa tunasema kitaalamu kuwa spishi hazina utulivu zinatapatapa.”

Hata hivyo, changamoto na athari za ukame zimeishusha idadi ya mbwa mwitu wa Afrika kwa zaidi ya nusu, Nyumbu ,nyati na paa aina ya Hirola. Yote hayo yakiendelea, ripoti hiyo pia imebainisha kuwa idadi ya twiga imeongezekea kutokea 35,555 mwaka 2021 hadi 43,000. Mafanikio hayo yameshuhudiwa pia kwenye idadi ya faru weusi na weupe ambao kila aina hiyo wamepita alfu moja.

Tathmini ya wanyamapori hufanyika kila baada ya miaka mitatu nchini Kenya kubaini idadi, hali ya mazingira na mawimbi ya jinsi wanavyohama.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW