1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaLibya

Idadi ya vifo yaongezeka kufuatia mafuriko Libya

24 Septemba 2023

Takriban wiki mbili baada ya mafuriko makubwa yaliyoharibu mji wa bandari wa Derna nchini Libya, idadi ya vifo inaendelea kuongezeka na sasa imefikia jumla ya watu 3,845.

Libyen Darna Mann sitzt in den Trümmern
Picha: KARIM SAHIB/AFP

Hayo yameelezwa na Mohamed Eljarh, msemaji wa kamati ya misaada iliyoundwa na serikali ya mashariki mwa Libya, ambaye amesisitiza kuwa idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka. Amesema idadi hiyo ni pamoja na wale tu ambao mazishi yao yameorodheshwa na wizara ya afya.

Mashirika ya kimataifa ya misaada yanasema huenda watu 10,000 au zaidi wamefariki kufuatia mafuriko hayo nchini Libya. Wengi wa waliofariki wanaaminika kusombwa na maji hadi baharini, Wengine wanadhaniwa kufukiwa chini ya vifusi katika vitongoji vyote vya Derna.

Soma pia: Idadi ya vifo vya mafuriko ya Libya yafikia 3,753

Shirika la Kimataifa la Uhamiaji IOM limesema mapema wiki hii kuwa zaidi ya watu 43,000 wameyakimbia makazi yao kutoka mji huo na maeneo jirani ya mashariki mwa Libya.