1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya wahamiaji Italia yaongezeka

Isaac Gamba13 Aprili 2016

Idadi ya wahamiaji wanaowasili Libya kwa lengo la kuvuka Bahari ya Mediterranea imeanza kuongezeka na hivyo Umoja wa Ulaya kuitahadharisha Italia kujiandaa kukabiliana na wakimbizi watakaoingia nchini humo.

Wakimbizi wakivuka bahari kufika Ulaya
Picha: picture alliance/dpa/ Italian Navy Press Office

Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Donald Tusk alilieleza bunge la Ulaya akithibitisha kuanza kuibuka upya kwa wimbi hilo la wakimbizi nchini Libya ikiwa ni siku moja baada ya Austria kusema ilikuwa inapanga kuongeza udhibiti katika mpaka wake na Italia ili kukabiliana na wakimbizi wanaotarajiwa kuongezeka wakati wa majira ya kiangazi.

Tusk ameyataka mataifa yanayounda umoja huo kuwa tayari kukabiliana na idadi mpya ya wakimbizi watakaokuwa wakiwasili nchini Italia na Malta licha ya hatua ambazo tayari zimeanza kuchukuliwa na Umoja wa Ulaya za kujaribu kupunguza wakimbizi wanaoingia barani humo kufuatia kuanza kwa utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya Uturuki na Umoja wa Ulaya ya kuwarejesha Uturuki wakimbizi waliokuwa katika visiwa vya Ugiriki.

Naye Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Junker alilieleza bunge la Ulaya kuwa utekelezaji wa makubaliano kati ya Umoja huo na Uturuki bado ni suala ambalo linahitaji nguvu ya ziada kutokana na changamoto kadhaa zinazojitokeza ikiwa ni pamoja na umuhimu wa kulindwa kwa haki za bindamu ambapo Uturuki imekuwa ikinyooshewa kidole.

Askari wapambana na wakimbizi Macedonia

Kwa upande mwingine Donald Tusk amezitaka nchi wanachama wa umoja huo kushirikiana na Italia katika kukabiliana na wimbi hilo jipya la wakimbizi na kuonya kuwa endapo hakutakuwa na ushirikiano wa aina hiyo basi kuna uwezekano wa kujirudia kwa hali ya mwaka jana ambapo mataifa kadhaa barani Ulaya yalilazimika kufunga mipaka yake kufuatia kuongezeka kwa idadi ya wakimbizi ambao walikuwa wakijaribu kuvuka kupitia katika mipaka hiyo.

Alisema kuna haja ya kutorudia makosa yaliyofanyika mwaka jana ambapo kutokana na kuchelewa kuchukua hatua mapema za kushughulikia suala hilo ndio iliyosababisha baadhi ya mataifa yaliyoko katika mkataba wa Schengen kulazimika kufunga mipaka yao kwa muda ili kuzuia wakimbizi waliokuwa wakiingia katika mataifa hayo pasipo kufuata utaratibu wa kawaida.

Askari wazuia wakimbizi kuvuka mpaka eneo la IdomeniPicha: picture-alliance/AP Photo/A.Emric

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa Kiasi ya wakimbizi 10,000 waliwasili nchini Italia mwezi uliopita ukilinganisha na idadi ndogo ya wakimbizi 2,300 waliowasili nchini humo mwezi Machi mwaka 2015 huku idadi ya wahamiaji wanaowasili nchini Ugiriki ikipungua baada ya Uturuki kukubali kuwapokea wahamiaji wanaorejeshwa kutoka nchini Ugiriki wakiwemo wale wanaotoka nchini Syria.

Wakati huo huo mapambano yameibuka upya kati ya askari polisi wa Macedonia na wahamiaji waliokwama katika makambi ya wakimbizi kwenye mji wa mpakani wa Idomeni nchini Ugiriki. Picha zilionyesha polisi wakilazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi ili kukabiliana na watu waliokuwa wakijaribu kuvuka mpaka kwa nguvu kwa kuvunja uzio uliowekwa mpakani.

Kiasi ya wahamiaji 300 na polisi kadhaa walijeruhiwa Jumapili iliyopita katika tukio linalofanana na hilo wakati kiasi ya watu 3,000 walipokuwa wakijaribu kulazimisha kuvuka kuingia Macedonia baada ya kukwama kwa zaidi ya mwezi mmoja katika kambi hiyo ya Idomeni.

Mwandishi: Isaac Gamba/ DPAE/ RTRE

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW