1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki/Syria: Idadi ya watu waliokufa yapindukia elfu 30.

12 Februari 2023

Umoja wa Mataifa umelaani hatua ya kushindwa kufikisha msaada unaohitajika kwenye maeneo yanayokabiliwa na vita nchini Syria.

Türkei, Kahramanmaras | Erdbeben
Picha: Ismail Coskun/IHAAP/AP/picture alliance

Mkuu wa kitengo cha misaada cha Umoja wa Mataifa Martin Griffiths amesema hadi sasa imeshindikana kuwafikia watu wa kaskazini-magharibi mwa Syria. Ameeleza msafara wa magari ya Umoja wa Mataifa yaliyobeba vifaa kuelekea kaskazini magharibi mwa Syria umewasili kupitia Uturuki kwa ajili ya mamilioni ya watu ambao nyumba zao ziliharibiwa na mitetemeko iliyotokea lakini imechelewa kufika Syria.

Msafara wa magari ya Umoja wa Mataifa yaliyobeba msaada katika mpaka wa Bab al Hawa.Picha: OMAR HAJ KADOUR/AFP

Syria kwa miaka mingi inakabiliwa na migogoro hali ambyo imesababisha kuzorota kwa utoaji wa huduma za afya huku baadhi ya sehemu katika nchi hiyo zinaendelea kudhibitiwa na  waasi wanaopambana na serikali ya Rais Bashar al-Assad, ambayo imewekewa vikwazo nan chi za Magharibi.

Soma:Uturuki-Syria: Idadi ya vifo yaongezeka na kufikia 28,000

Kwa mujibu wa mwandishi wa shirika la habari la AFP, msafara wa malori kumi ya Umoja wa Mataifa ulivuka kuelekea kaskazini-magharibi mwa Syria kupitia mpaka wa Bab al-Hawa, ukiwa umebeba matunubari, mablanketi, magodoro, mazulia na vifaa vingine.

Wakati huo huo maelfu ya waokoaji wanaendelea kuvifikia vitongoji vilivyoharibiwa na mitetemeko hiyo wakati ambapo baridi kali inaongeza huzuni kwa mamilioni ya watu wanaohitaji msaada.

Mji wa ulioharibiwa na tetemeko la ardhi wa Sarmada wa kaskazini magharibi mwa Syria. Picha: MUHAMMAD HAJ KADOUR/AFP/Getty Images

Watalaam wameeleza kwamba matumaini ya kuwapata watu walio hai katika vifusi yanafifia kadri siku zinavyopita. Lakini kuna Habari za kutia moyo pia kama za mtoto wa miezi saba anayeitwa Hamza aliyeokolewa kusini mwa jimbo la Hatay zaidi ya saa 140 baada ya tetemeko hilo. Mtoto mwingine Esma Sultan, mwenye umri wa miaka 13, aliokolewa katika mji wa Gaziantep, vyombo vya habari vya serikali vimeripoti.

Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis ametoa wito wa kutolewa msaada kwa waathiriwa wa tetemeko hilo, akiwataka watu kufikiria nini kinachoweza kufanyika ili kuwasaidia.

Soma:Rais Erdogan akiri shughuli za uokozi zinakwenda taratibu

Umoja wa Mataifa umesema takriban watu 870,000 wanahitaji haraka msaada wa chakula katika nchi za Uturuki na Syria. Hadi watu milioni 5.3 wamepoteza makazi yao nchini Syria. Takriban watu milioni 26 wameathiriwa na tetemeko hilo la ardhi. Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema limeomba dola milioni 42.8 ili kukabiliana na mahitaji ya haraka ya afya baada ya hospitali nyingi kuharibiwa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: SNA/IMAGO

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelihimiza Baraza la Usalama kuidhinisha kufunguliwa kwa vituo vipya vya misaada kwenye mipaka kati ya Uturuki na Syria, na ametaka ufanyike mkutano utakaoijadili Syria katika siku zijazo.

Vyanzo:AFP/DPA

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW