1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya waliofariki yafikia watu 50 New Zealand

Sekione Kitojo
17 Machi 2019

Watu wa New Zealand walimiminika katika maeneo ya kumbukumbu na kuweka maua na kuomboleza wahanga wa mauaji katika misikiti miwili leo Jumapili (17.03.2019),kukiwa na  ushahidi wa ujasiri wa kutukuka katika kadhia hiyo.

Terroranschlag Neuseeland Trauer Christchurch
Picha: picture-alliance/dpa/M. Tsikas

 Wakati hayo  yakifanyika  ushahidi  ulijitokeza wa ujasiri wa kutukuka pamoja na machungu ya mateso katika  mashambulio ya bunduki ambayo yalichukua  maisha  ya  watu 50.

Kijana akiomboleza mbele ya lundo la maua katika eneo la tukio la mauaji mjini ChrstchurchPicha: picture-alliance/dpa/Kyodo

Kamishna  wa  polisi Mike Bush  amesema  maafisa  hatimaye waliweza  kuwapatia  familia  orodha  ya  wahanga, kitu kilichocheleweshwa  kutokana  na  haja  ya  kazi  ya  tahadhari  ya polisi  pamoja  na  kiwango cha  mkasa  huo. Kwa  muda  wa  karibu siku  tatu timu za uchunguzi  wa  alama  katika  matukio ya  uhalifu , wengi  wakiwa  wamekuja  kutoka  sehemu  mbali  mbali  za  New Zealand , wamekuwa  wakifanyakazi  katika  maeneo  kadhaa  ya uhalifu, katika  misikiti  ya  Al Noor  na  Linwood  pamoja  na  nyumba katika  eneo  la  Dunedin, mji wa  kusini  mashariki  ambako  mtu anayeshukiwa  kuwa  ndie  aliyefanya  mashambulizi  ya  bunduki , aliishi.

Miili ya  wale  waliopigwa  risasi  na  mtu  huyo mwenye imani  ya kuwa  jamii  ya  wazungu ndio bora  zaidi iliendelea  kubakia  ndani ya  msikiti  ikisubiri uchunguzi wa  kitaalamu na  utambuzi wa wanafamilia  ambao  wamekuwa  katika  hali  ya  kufadhaika  mno ambao  wanataka  haraka  kuanza  taratibu  za  mazishi.

Tayari , matrekta  ya  kuchimba  yameanza  kazi  katika  eneo  la makaburi  mjini  humo  kuondoa  mchanga  unaohitajika  kwa  ajili  ya kuwazika wahanga waliofariki.

Mara  utambulizi utakapokamilika  majina yatatangazwa, Bush alisema. Lakini  tayari , taarifa  za  wahanga  kutoka  katika  mataifa ya  Kiislamu zimeanza  kuonekana.

Mwanamke akiwa katika majonzi makubwa katika eneo la kumbukumbu ya mauaji mjini ChristchurchPicha: picture-alliance/dpa/Kyodo

Mtoto mdogo yuko mahututi

Maafisa  wa  New Zealand  wamesema  watu 34  wanaendelea kuwapo  Hospitali, wakitibiwa majeraha  ambayo  daktari Greg Robertson alielezea   kuwa  ni  kutoka  hali  mbaya, majeraha ambayo yana ugumu  wa  kutibika  kutokana  na  risasi, hadi "majeraha madogo  madogo".

Miongoni  mwa  wale  ambao wanatapia  maisha  yao  ni  pamoja  na mtoto  wa  miaka  minne Alin Alsati.

Mtoto  huyo ambaye  yuko  katika shule ya  chekechea alikuwa anasali  kandoni  mwa  baba  yake Waseeim katika  msikiti  wa  Al Noor wakati  aliposhambuliwa  kwa  risasi karibu  mara  tatu. Alipelekwa  katika hospitali  ya  watoto  ya  Starship  mjini  Auckland kwa  helikopta, ikiwa  ni  hospitali  ya  juu  nchini  humo  ya  kituo cha mifupa. Baba  yake , ambaye  pia  alipigwa  risasi, alihamia  hivi karibuni  nchini  New Zeland  kutoka  Jordan na  alikuwa  ameanzisha duka  la  kinyozi , katika  kitongoji cha  Richmond.

"Tafadhali  niombeeni na  mtoto  wangu  wa  kike," alitoa  rai  hiyo katika ujumbe  wa  vidio katika  ukurasa  wa  Facebook akiwa hospitali  kabla  ya  kufanyiwa  upasuaji kuondoa  vipande vya  risasi na  mfupa  katika  eneo  lake  la  kiuno.

Polisi wakifanya ukaguzi katika eneo la tukio la mashambulizi mjini ChristchurchPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Baker

Mjini  Christchurch, New Zealand  na  duniani  kwa  jumla  kumekuwa na  mikesha, sala, kumbukumbu  na  ujumbe wa  mshikamano.

"Tuko  pamoja na  ndugu  zetu  Waislamu," ni  maneno  katika  bango kubwa  jekundu miongoni  mwa  maua mengi  yaliyowekwa  katika sehemu  moja  katika  kile  wakaazi  waliochosema  kuwa  ni "mji wa huzuni".

Katika "kanisa  kuu  la mbao"  mjini  Christchurch, lililojengwa  baada ya   tetemeko  la  ardhi  la  mwaka 2011 ambalo bado  limeweka  doa katika  mji  huo , Dean Lawrence Kimberley aliendesha  misa  katika kuonesha "mshikamano na  jamii  ya  waislamu."

"Tumejifunza  wakati  wa  tetemeko  kwamba  katika  wakati  wa majaribu  ni  vizuri  kunyoosheana  mikono. Muda ni  muafaka  wa kufanya  hivyo  tena,"  amewaambia  waumini.

Wakaazi waomboleza

Mjini Auckland , wakaazi  wa  jamii  zote  waliokuwa wakititikwa  na machozi  walisimama  wakishikana  mikono  nje  ya  msikiti  wa Umar kutoa heshima  zao.

Katika  eneo  la  bahari  ya  Tasmin , Waaustralia  waliopatwa  na mshituko kwamba  kitendo  kama  hicho  katika  taifa  hilo  ndugu kimefanywa  na  mmoja  wao, waliapa kutoa  msaada  wowote ule wanaoweza.

Jengo maarufu la Opera mjini Sydney likiwa na tawi la fedha alama ya New ZealandPicha: Getty Images/J. D. Morgan

Mjini  Sydney , tawi la fedha , ishara  ya  New Zealand, iliwekwa katika sehemu  ya  jengo  la  maarufu  duniani  la  Opera.

Siku  ya  Jumamosi Tarrant  alifikishwa  mahakamani mjini Christchurch  kukabiliwa  na  kile  kinachotarajiwa  kuwa  moja  kati ya  mashitaka  kadhaa  ya  mauaji.

Akisindikizwa  na  polisi  wenye  silaha, mkufunzi  huyo wa  zamani wa viungo  alionesha  ishara ya "okay" iliyopinduliwa ikiwa  ni  ishara inayotumiwa  na  makundi  ya  imani  za nguvu  ya  uzungu  duniani kote.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe

Mhariri: John Juma

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW