1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waliokufa kufuatia maporomoko ya ardhi Tanzania wafikia 68

5 Desemba 2023

Idadi ya waliofariki katika maporomoko ya udongo kufuatia mvua kubwa iliyonyesha nchini Tanzania imefikia watu 68 huku wengine 116 wakiripotiwa kujeruhiwa.

Tansania Erdrutsch Katesh
Picha: Xinhua/picture alliance

Hayo yameelezwa na Queen Sendiga, mkuu wa mkoa wa Manyara uliokumbwa na maafa hayo. Kikosi cha wataalam wapatao 350 kutoka jeshini kimetumwa eneo hilo kusaidia zoezi la uokozi. 

Rais wa Tanzania, Samia suluhu Hassan ametangaza kuwa serikali yake itagharamia mazishi ya wale waliopoteza maisha kutokana na maafa hayo.

Athari ya mvua katika mataifa mengi ya Afrika Mashariki

Mvua kubwa ilinyesha siku ya Jumamosi jioni na kusababisha maporomoko ya udongo kwenye mlima Hanang. Mji wa Katesh, ulio chini ya mlima huo uliathiriwa pakubwa. Nchi nyingi za Afrika Mashariki zimekuwa zikikumbwa kwa wiki kadhaa na mvua kubwa na mafuriko yanayohusishwa na El Niño.

Soma zaidi:Takriban watu 47 wamekufa Tanzania kufuatia maporomoko ya ardhi

Taasisi yenye kuhusika na Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA), inasema zaidi ya watu 200 wamepoteza maisha nchini Kenya na Somalia pekee. Mamilioni ya watu walilazimika kukimbia vijiji na miji yao. Mvua hiyo kubwa inatokea katika kipindi kifupi baada ya eneo la Pembe ya Afrika kukumbwa na  ukame mkali zaidi.

Chanzo: DPA

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW