1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaAfrika

Idadi ya waliokufa kwa tetemeko Morocco yazidi watu 2,000

10 Septemba 2023

Morocco inaomboleza vifo vya zaidi ya watu 2,000 vilivyosababishwa na tetemeko kubwa la ardhi lililotokea Ijumaa usiku, wakati timu za uokoaji zikifanya juhudi kuwatafuta watu waliokwama kwenye vifusi.

Athari za tetemeko la ardhi Morocco
Athari za tetemeko la ardhi MoroccoPicha: Abdelhak Balhaki/Reuters

Wanajeshi na wafanyakazi wa kutoa misaada wameonekana wakipeleka maji na mahitaji mengine katika vijiji vilivyoathiriwa.

Janga hilo, hadi sasa limesababisha takribani watu wengine wasiopungua 2,000 kujeruhiwa wengi wao wakiwa katika hali mbaya kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni huku idadi hiyo na ya vifo ikitarajiwa kuendelea kuongezeka.

Tetemeko hilo la ardhi lenye ukubwa wa 6.8 kwa kipimo cha Richter lilitokea umbali wa kilomita 72 kusini magharibi mwa mji wa kitalii na wakihistoria wa Marrakech ambapo liliviharibu vijiji vingi. Familia nyingi katika mji wa Marrakech zimelala nje kwa usiku wa pili baada ya mkasa huo zikihofia kuwa nyumba zao hazina tena usalama. 

Sehemu ya uharibifu uliotokana na tetemeko la ardhi mjini MarrakechPicha: Al Oula TV via REUTERS

Mamlaka nchini humo zimetangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa wakati mataifa mengine yakiwemo Israel, Ufaransa, Uhispania, Italia na Marekani yametangaza kutoa msaada. Taifa jirani la Algeria ambalo limekuwa na uhusiano wa mashaka na Morocco lilifungua anga yake ambayo liliifungia Morocco kwa miaka miwili, ili kuruhusu ndege zinazobeba misaada ya kiutu na majeruhi ziweze kulitumia.

Itachukua miaka kadhaa kukarabati maeneo yaliyoathiriwa

Mkurugenzi wa Shirika la Msalaba Mwekundu katika Mashariki ya kati na Kaskazini mwa Afrika Hossam Elsharkawi amesema katika taarifa yake kuwa, huenda ikachukua miaka kadhaa kukarabati uharibifu uliotokea.

Kulingana na shirika la habari la AFP, kijiji cha Tafeghaghte, kilicho umbali wa kilometa 60 kusini magharibi mwa eneo lilipoanzia tetemeko hilo karibu chote kimeharibiwa vibaya. Ni majengo machache pekee yaliyosalia kijijini hapo.

Waathiriwa wa tetemeko la ardhi Morocco wakiwa wamelala nje Picha: Said Echarif/AA/picture alliance

Mmoja wa wakaazi, Moulay Brahim ambaye mkewe na watoto wanne wamefariki dunia katika tetemeko hilo amenukuliwa akisema, "Nimepoteza kila kitu, sina la kufanya sasa, ninataka tu kujificha mbali na dunia niomboleze".

Mkaazi mwingine wa kijiji hicho Omar Benhanna mwenye miaka 72, amesema "Wajukuu wangu watatu na mama yao wamekufa. Bado wamefunikwa na kifusi . Tulikuwa tunacheza sote muda si mrefu."  Wakaazi wa kijiji hicho, jana Jumamosi waliwazika watu 70 waliokufa kutokana na tetemeko hilo.

Jumamosi, wizara ya mambo ya ndani ya Moroccoilisema kuwa mamlaka zinafanya mipango ya kuharakisha operesheni za uokoaji ili kuwanasua watu waliojeruhiwa.

Tetemeko hilo ni baya zaidi kuwahi kutokea Morocco tangu lile la mwaka 1960 lililouharibu vibaya mji wa Agadir na kusababisha vifo vya watu 12,000 ambao walikuwa theluthi moja ya idadi jumla ya watu mjini hapo kwa wakati huo

  

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW