1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya waliokufa kwenye shambulio nchini Congo yafikia 8

27 Desemba 2021

Idadi ya watu waliopoteza maisha katika shambulio la bomu la siku ya Krismasi katika mji wa Beni mashariki mwa Kongo, imeongezeka na kufika watu wanane.

Symbolbild | DR Kongo | Anschlag der Alliierte Demokratische Kräfte Kongo
Wanajeshi wa Kongo FARDC wakiwasaka waasi wa ADF kufuatia shambulio BeniPicha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Mamlaka ya mji wa Beni yamerefusha muda wa marufuku ya kutotoka nje usiku, katika juhudi za kukabiliana na kundi la waasi la ADF linalotuhumiwa kufanya shambulizi hilo kwenye mgahawa.

Tangu kuanzishwa kwa operesheni za pamoja kati ya jeshi la Congo FARDC na lile la Uganda UPDF novemba thelathini, hasa katika eneo la mashariki ya Beni, waasi wa ADF wamezidisha  mashambulizi yao katika maeneo ya Kaskazini pamoja na magharibi ya Beni.

Kila uchao, wakaazi wa wilaya ya Beni katika mkoa wa Kivu ya Kaskazini, Irumu pamoja na Mambasa katika mkoa wa Ituri, wamekuwa wakishuhudia mashambulizi ya waasi hao, wanaowauwa watu, kuchoma magari, pikipiki pamoja na nyumba.

Kijiji kinichoshuhudia shambulizi wikendi iliopita ni kile cha Kabalwa katika secta ya Ruwenzori, ambako mkaazi mmoja aliuawa na wengine wawili kuchukuliwa na ADF pamoja na kuchoma maduka baada ya kuyapora.

Mamlaka ya mji wa Beni yamerefusha muda wa marufuku ya kutotoka nje usiku

Wanajeshi wa jeshi la Kongo wakipiga doria katika kijiji cha ManzalahoPicha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Mashambulizi yote hayo yanafanywa na ADF, ngome zake mbili muhimu zimetekwa na majeshi ya muungano, yaani kambi ya Jua namba moja na Kambi ya Jua namba mbili, mbunge Kiro Tsongo Grégoire mchaguliwa wa Beni mjini, anaomba vyombo vya usalama kuimarisha usalama katika maeneo makubwa makubwa,ilikuzuia mashambulizi ya ADF.

"Kwenyi miji na vijiji kunapashwaimarishwa usalama. Maeneo kama Beni mjini,kama Kasindi, Oicha, Bulongo ambako kuna wakaazi wengi, yanapaswa kulindwa kupitia pia doria na kuweka vizuizi katika kona zote ilikukagua watu wanaoondoka na wanaoingia. Na katikati ya maeneo hayo, inabidi kulinda usalama kwenyi maeneo yanayotembelewa zaidi."

Idadi ya wahanga wa shambulizi la juzi jumamosi mjini Beni imeongezeka.

Ni watu wanane sasa waliopoteza maisha yao, katika shambulizi la kigaidi lililolenga mgahawa Inbox siku ya Krismasi.

Idadi hiyo huenda ikaongezeka kufuatia hali ya majeruhi ambayo sio nzuri kwa baadhi yao.

Shambulizi hilo la kigaidi mjini Beni, limepelekea Gavana wa jeshi kurefusha muda wa marufuku ya kutoka nje katika mji wa Beni.

Ifikapo saa moja usiku, wakaazi wote wa Beni wanatakiwa kubaki makwao, jambo litakalosaidia vyombo vya usalama kutekeleza majukumu yao ipaswavyo, alisema Jenerali Ndima Kongba Constant, gavana wa mkoa wa Kivu ya Kaskazini.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW