Idadi ya waliouawa Burkina Faso yafikia watu 79
14 Juni 2022Idadi ya vifo vilivyotokana na mauaji yaliofanywa na watu wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa itikadi kali kaskazini mwa Burkina Faso mwishoni mwa juma lililopita imeongezeka hadi 79.Jeshi laahidi kurejesha usalama Burkina Faso
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na serikali siku ya Jumanne, "miili 29 zaidi imepatikana. Idadi hii inaongeza katika miili 50 ambayo tayari ilikuwa imepatikana na kufanya idadi ya wahanga wa mauaji hayo kufikia 79."
Shambulio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Jumamosi katika kijiji cha Seytenga. Kijiji hicho kilishuhudia mapigano wiki iliyopita ambayo yaliua askari 11, na kusababisha operesheni ya kijeshi ambayo jeshi lilisema ilisababisha vifo vya karibu wanajihadi 40.
Kiongozi wa kijeshi wa taifa hilo Paul-Henri Sandaogo Damiba, alitangaza amri siku ya Jumatatu akiamuru nchi nzima kufanya maombelezo ya siku tatu hadi usiku wa Alhamis.
"Bendera zitapepea nusu mlingoti katika majengo ya umma na katika balozi za Burkina Faso", ilisema amri hiyo inayopiga marufuku maadhimisho na mikusanyiko ya burudani. Amri ya Kamanda Damiba ilielezea washambuliaji "kama watu wasiojulikana wenye silaha".
Taifa hilo la kanda ya Sahel limekabiliwa na uasi wa miaka saba ambao umegharimu maisha ya watu zaidi ya 2,000 na kulazimisha wengine kiasi cha karibu milioni 2 kuyakimbia makaazi yao.
Umoja wa Ulaya ulionya kwamba shambulio hilo linaweza kuwa limewaua "zaidi ya wahanga wa kiraia 100" na kulaani tukio hilo, na kutaka uchunguzi zaidi juu ya mauaji hayo.Burkina Faso kukabiliwa na hali tete zaidi?
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell alisema kuwa "njia iliyotumiwa na kundi la kigaidi ambalo lilitekeleza shambulio hilo, yaani unyongaji wa kila mtu waliyekutana naye katika kijiji hicho ni ya kutisha."
Uasi wa wanamgambo umeshamiri katika eneo la kaskazini mashariki mwa Burkina Faso, ukiongozwa na wavamizi wanaoshukiwa kuwa na uhusiano na makundi ya Al-Qaeda au lile linalojiita Dola la Kiislamu IS.