1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya waliouwawa katika mapigano nchini Somalia yaongezeka

Mwakideu, Alex21 Aprili 2008

Mashekhe tisa miongoni mwa waliouawa katika mapigano ya mwishoni mwa wiki

Wanamgambo wa kiislamu wakiongea na raia wa SomaliaPicha: AP

Idadi ya waliouwawa katika vita kati ya wanamgambo wa kiislamu na wanajeshi wa Somalia wanaoshirikiana na wa Ethiopia imeongezeka na kufikia watu 85.


Kufuatia mapigano hayo Ehtiopia imekata uhusiano wake na Qatar ikidai kwamba nchi hiyo inafadhili ugaidi nchini Somalia na pia katika zingine za Pembe ya Afrika.


Mji mkuu wa Somalia Mogadishu umeshuhudia mapigano makali zaidi katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.


Miili ya watu waliouwawa katika mapigano hayo yaliyoanza jumamosi ingali katika bara bara za mji huo. Wanajeshi wanne wa Somalia wameuwawa na wengine saba wakajeruhiwa kabla wanamgambo wa kiislamu kuuteka mji wa kusini wa Guda.


Miili mitatu ya mashekhe imepatikana kando ya msikiti wa Al-Hidaya na mingine sita ndani ya msikiti huo ulioko kaskazini mwa Mogadishu.


Mkaazi wa eneo hilo Farah Fargan amesema mashekhe hao waliuwawa na majeshi wa Ethiopia. Sheikh Mohamed Muse aliyeshuhudia mapigano hayo amesema majeshi hao baadaye waliwakamata vijana 21 waliokuwa wanajificha ndani ya msikiti huo.


Mapigano ya mwishoni mwa wiki yalishuhudiwa zaidi katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo.

Hussein Abdulle ambaye alikuwa anajaribu kutoroka mapigano hayo akihofia kwamba yataanza tena amesema ameona miili ya watu wane anaowajua.


Mkaazi mwengine Abdulahi Mahamud amesema ameona takriban watu ishirini wengi wao wanawake na watoto wakijificha katika msikitini unaolindwa na majeshi ya Ethiopia.


Katika miezi ya hivi karibuni wanamgambo wa kiislamu wamekuwa wakishambulia miji midogo midogo na kuiteka kutoka mikononi mwa walinda usalama wanaoshirikiana na serikali. Hata hivyo wamekuwa wakitoweka baada ya usaidizi wa kijeshi kuitishwa katika miji hiyo.


Wadadisi wanalitaja kundi la wanamgambo la al Shabaab kama kundi linalohusika na mashambulio hayo.


Mwezi uliopita Marekani ililiingiza kundi la al Shabaab katika orodha ya makundi ya kigaidi duniani.


Wanamgambo wa kiislamu wameuteka mji mwengine wa Dinsor na kuanzisha sheria za kiislamu katika eneo la Wajid.


Mmoja wa wakaazi wa eneo hilo Aden Abdirahman amesema wanamgambo hao wamewaonya dhidi ya utafunaji miraa, uvutaji sigara, kutazama sinema au kuondoa vizuizi vya barabarani.


Mwaka wa 2006 serikali ya mpito ya Somalia inayoongozwa na Rais Abdullahi Yusuf ilifanikiwa kuwafurusha wanamgambo wa kiislamu kutoka mjini Mogadishu. Hata hivyo serikali hiyo imekuwa ikikabiliwa na mashambulio ya mara kwa mara sawa na yale yanayoshuhudiwa nchini Iraq.


Mgogoro wa Somalia umepelekea nchi hiyo kuwa na takriban wakimbizi milioni moja ndani yake.


Kwa upande mwengine polisi wamemkamata mhariri wa kituo cha redio cha Shabelle kwa mashtaka ya kutangaza habari za uongo kuhusu vita hivyo.


Kamanda wa polisi Abdulkadir Mohamed amesema mwanahabari huyo aliripoti kwamba wanamgambo wa kiislamu wameshambulia na kuteka uwanja wa Gulwade ilhali polisi wangali katika uwanja huo na hakuna mapigano yaliyotokea mahala hapo.


Shirika la Elman Peace and Human Rights Organisation, linalofuatilia mapigano hayo likiwa nchini Somalia limeripoti kuuwawa kwa watu 81 na kujeruhiwa kwa wengine 119.


Watafiti wanakadiria kwamba watu 6,500 waliuwawa mwaka uliopita mjini Mogadishu pekee na wengine milioni moja na laki tano wakaachwa bila makao.


Wafanyikazi wa misaada wanasema raia 250,000 wanaishi katika makaazi ya mda nje ya mji wa Mogadishu; jambo linaloifanya Somalia kuwa nchi inayoongoza kwa raia wanaoishi kama wakimbizi nchini mwao.


Somalia imekuwa katika hali ya mapigano ya mara kwa mara tangu mwaka wa 1991 alipog'atuliwa mamlakani Rais wa zamani wa nchi hiyo Said Bare.


Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW