1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya waliouwawa Kenya huenda ikapanda

4 Aprili 2015

Idadi ya watu waliouwawa katika shambulio lililofanywa na wanamgambo wa Somalia dhidi ya chuo kikuu nchini Kenya huenda ikapanda na kufikia zaidi ya watu147,duru za serikali pamoja na vyombo vya habari zimesema.

Kenia Garissa Universität Anschlag Trauer
Baadhi ya wanafunzi wakiwa na majonzi kuwapoteza wenzaoPicha: Reuters/Herman Kariuki

Hasira miongoni mwa wakaazi wa eneo hilo imepanda kuhusiana na kile wanachosema kuwa ni kushindwa kwa serikali kuzuia umwagikaji huo wa damu.

Wakiwa wamejifunga miripuko, wapiganaji waliokuwa wamefunika nyuso zao wa kundi la al-Shabaab walikivamia chuo kikuu cha Garissa, kiasi ya kilometa 200 kutoka mpaka wa Somalia, katika shambulio lililofanyika alfajiri siku ya Alhamis.

Wanafunzi wa chuo kikuu mjini Garissa wakibembelezana baada ya shambulio dhidi ya chuo hichoPicha: Reuters/Herman Kariuki

Wakirusha maguruneti na kufyatua risasi ovyo katika kundi la wanafunzi, washambuliaji awali waliua kila mtu aliyekuwapo karibu. Lakini baadaye waliwawatenga baadhi ya Waislamu na badala yake wakawalenga wanafunzi Wakristo katika mzingiro huo chuoni hapo uliodumu kwa masaa 15.

Hasira zimeongezeka

Hasira kufutia mauaji hayo zimeongezwa na ukweli kwamba kulikuwa na tahadhari wiki iliyopita kwamba shambulio kama hilo dhidi ya chuo kikuu litafanyika. Wakaazi wanawashutumu maafisa kwa kutofanya vya kutosha kuimarisha ulinzi katika eneo hilo ambalo halijapata maendeleo ya kutosha.

Watu watano wamekamatwa kwa kuhusika na shambulio hilo, kimeripoti kituo cha televisheni cha CNN jana Ijumaa (03.04.2015), kikimnukuu waziri wa mambo ya ndani nchini Kenya Joseph Nkaissery.

Wanajeshi wakilinda lango la kuingia katika chuo hicho mjini GarissaPicha: Reuters/Noor Khamis

"Ni kutokana na kubweteka kwa serikali ambapo mambo kama haya yanatokea. Kwa kitu kama hiki kutokea wakati kulikuwa na uvumi haikubaliki," amesema Mohammed Salat , mwenye umri wa miaka 47, mfanyabiashara mwenye asili ya Somalia , raia wa Kenya.

Maafisa wanasema karibu watu 150 wameuwawa, na kiasi ya wengine 79 wamejeruhiwa, wengi wao wakiwa katika hali mbaya. Lakini kwa kuwa kuna idadi isiyojulikana ya wanafunzi na waalimu ambao hawajulikani waliko, idadi ya waliouwawa inaweza kupanda.

Kundi la al-Shabaab limetishia kufanya mashambulizi mapya nchini Kenya jana Ijumaa huku serikali ya Kenya ikitangaza kufungwa kwa chuo kikuu hicho ambacho wapiganaji hao wa Kisomali walifanya shambulio lao baya kabisa hadi sasa.

Wakenya hawatakuwa na usalama

"Hakutakuwa na mahali salama kwa Wakenya wakati majeshi yao yako nchini Somalia," msemaji wa al-Shabaab Sheikh Ali Mohamud Rage ameiambia redio inayounga mkono mapambano ya wapiganaji hao Andalus.

Wanafunzi wakiwa bila mashati katika chuo kikuu cha GarissaPicha: picture-alliance/AP Photo

Kenya inashiriki katika kikosi chenye wanajeshi 20,000 cha Umoja wa Afrika ambacho kinaisaidia serikali ya Somalia kupambana na kundi la al-Shabaab.

"Mtaona mashambulizi zaidi mabaya nchini mwenu, Kenya," Rage amesema baada ya shambulio la siku ya Alhamis , katika chuo kikuu cha Moi mjini Garissa.

Nje ya lango kuu la kuingia chuoni hapo, wanawake kadhaa waliojifunga hijabu wanamatumaini kwamba watu ambao hawajulikani walipo watajitokeza wakiwa hai.

Ghasia hizo zitaongeza mbinyo zaidi kwa Rais Uhuru Kenyatta , ambaye amesumbuka kuzuia mashambulizi ya watu wenye silaha pamoja na mashambulizi ya maguruneti hali ambayo imechafua heba ya Kenya nje ya nchi na kusababisha sekta muhimu nchini humo ya utalii kufikia hali ya kuporomoka kabisa.

Jana Ijumaa Rais wa Marekani Barack Obama amempigia simu rais Kenyatta na kutoa rambi rambi zake kutokana na shambulizi hilo aliloliita la waoga na kuthibitisha kwamba bado anapanga kufanya ziara nchini humo baadaye mwaka huu, imesema Ikulu ya Marekani ya White House.

Wanajeshi wakilinda doria mjini Garissa nchini KenyaPicha: E. Ndikumana/AFP/Getty Images

Zaidi ya watu 400 wameuwawa na kundi hilo al-Shabaab lenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda katika taifa hilo la Afrika mashariki tangu Kenyatta alipoingia madarakani Aprili mwaka 2013, ikiwa ni pamoja na watu 67 ambao wameuwawa katika jumba la maduka la Westgate katika mji mkuu Nairobi Septemba mwaka huo.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / dpae

Mhariri: Caro Robi

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW