Idadi ya watoto wanaofanya umachinga yaongezeka Uganda
1 Septemba 2020Huku baadhi ya wazazi wakielezea kuwa ni vyema watoto wajifunze njia za kuingiza kipato, wengine wanahofia kuwa hii itasababisha watoto wengi kuacha masomo kwani sasa wanavutiwa zaidi na mazoea na kupata pesa na kuwa na uhuru wa kufanya vile wapendavyo.
Hali kama hii inashuhudiwa hata katika miji mingine ya Uganda ikiwemo Jinja, Mbarara, Mbale, Gulu na kwingineko.
Hapo awali kabla ya shule kufungwa kutokana na hatua za kudhibiti kuenea kwa COVID-19, idadi ya watoto waliokuwa wakishiriki biashara hii walikuwa wachache sana. Watoto hao wanauza vitu mbalimbali kama vile matunda, vitafunio na vitu vingine vya matumizi ya nyumbani.
Kwa upande wao, watoto walio kati ya umri wa miaka saba hadi 16 wanaeleza kuwa wamelazimika kushiriki biashara hii ya umachinga kwa sababu wengi wa wazazi wao walisimamishwa kazi na hii ndiyo njia ya pekee kujikimu kama familia.
Mmoja kati ya watoto amesimulia kuwa akirudi nyumbani bila kupata kiasi fulani cha pesa anaadhibiwa na wazazi wake na ndiyo maana yeye hurauka kuja kuuza ndizi na kuondoka jioni kuelekea usiku ili angalau atimize maagizo ya wazazi wake.
Masaibu mengine yanayowakumba watoto hao ni pale makundi ya waporaji kwenye barabara hizo za miji wanapowavamia na kuwapokonya pesa za mauzo yao.
Soma zaidi: Mkakati mkali wa Uganda wafanikiwa kudhibiti COVID
Lakini hoja kuu kuhusiana na mustakabali wa watoto hao ni hofu na mashaka kwamba watoto hao wataamua kuacha masomo kwa sababu wamezoea kuingiza pesa na kufanya vile wapendavyo kama vile kujifunza uraibu wa kunywa pombe na kuvuta sigara.
Baadhi ya wazazi na walimu wana mtazamo kuwa watoto hao watakaporudi shuleni, walimu watakabiliwa na changamoto kubwa kuwarudisha katika nidhamu waliokuwa nayo hapo awali.
Kufuatia kufunguliwa kwa sehemu mbalimbali za umma kwa shughuli za biashara na starehe, pamekuwepo na mwito shule pia zifunguliwe.
Wazazi wanaelezea kuwa hiyo ndiyo njia ya pekee kuweza kuwadhibiti watoto wao wasijihusishe katika mienendo itakayowasababisha kusahau masomo.
Yamkini Rais Museveni anakubaliana na wazo hilo pale aliposema kuwa makundi ya watu yanaweza kuzingatia kanuni za kuepusha kusambaa kwa virusi vya Corona katika mazingira ya nidhamu.
Akielezea masikitiko yake kuhusu idadi kubwa ya watoto wanaoshiriki umachinga, waziri nchi wa elimu Rosemary Senninde aidha anahofia kuwa walimu kadhaa pia wataacha taaluma hiyo.
Hii ni baada ya wao kugundua kuwa wanaweza kuingiza mapato bora katika biashara walizoanzisha katika kipindi hiki.
Serikali ilianzisha mpango wa wanafunzi kuendelea na masomo yao wakitumia redio na televisheni na pia kusambaza vitabu vya mazoezi. Lakini ni idadi ndogo sana ya wazazi na wanafunzi ambayo imezingatia fursa hii.