1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watoto wanaosajiliwa na magenge ya silaha waongezeka Haiti

Josephat Charo
25 Novemba 2024

Ongezeko la usajili wa watoto limechochewa na ongezeko la machafuko, umaskini, ukosefu wa elimu na miundombinu mibovu inayokaribia kusambaratika.

Magenge yanadhibiti sehemu kubwa ya mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince
Magenge yanadhibiti sehemu kubwa ya mji mkuu wa Haiti, Port-au-PrincePicha: Ralph Tedy Erol/REUTERS

Shirika linalowahudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF limetahadharisha kwamba idadi ya watoto nchini Haiti waliosajiliwa na magenge yenye silaha imeongezeka kwa asilimia 70 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Shirika hilo limeonya kwamba watoto wanakaribia aslimia 50 ya idadi jumla ya wanachama wa magenge hayo.

Haiti imehangaika kutokana na miongo kadhaa ya kuyumba kwa hali ya kisiasa, lakini katika miezi ya hivi karibuni nchi hiyo imeshuhudia ongezeko kubwa la machafuko huku magenge sasa yakidhibiti asilimia 80 ya mji mkuu Port-au-Prince.

Katika taarifa yake UNICEF imesema ongezeko hilo ambalo halikutarajiwa, lilirekodiwa robo ya pili ya mwaka 2023 na 2024 na linaashiria mgogoro wa ulinzi wa watoto unaoendelea kuwa mbaya nchini Haiti.