1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya watu waliokufa Indonesia yaongezeka hadi 1,407

Lilian Mtono APE, DPAE
3 Oktoba 2018

Msemaji wa idara ya kitaifa ya majanga Sutopo Nugroho amesema idadi ya wahanga kufikia hii leo ni 1,407

Indonesien Sulawesi nach dem Erdbeben
Picha: picture-alliance/AP Photo/T. Syuflana

Idadi ya watu waliokufa kufuatia matetemeko ya ardhi na Tsunami yaliyopiga kisiwa cha Sulawesi nchini Indonesia imeongezeka na kufikia 1,407 hii leo, huku watoa huduma za afya wakikabiliana na idadi kubwa ya majeruhi, katika wakati ambapo pia kuna tatizo la kukatika kwa umeme na upungufu wa mafuta. Aidha, katika kisiwa hicho pia kumeripotiwa mripuko wa Volkano katika mlima wa Soputan, uliotokea hii leo. 

Msemaji wa idara ya kitaifa ya majanga Sutopo Nugroho amesema idadi ya wahanga kufikia hii leo ni 1407. Ameongeza kuwa vifo hivyo vimetokea kuanzia maeneo ya Palu, Sigi, Donggala na Pargi-Moutong. Na kwamba tayari wamewazika watu 519 miongoni mwao.

Ameongeza kuwa zaidi ya watu 2,550 waliojeruhiwa vibaya wameendelea kupata matibabu hospitalini, huku wengine 113 wakiwa hawajulikani walipo baada ya janga hilo la tetemeko lililotokea Ijumaa iliyopita.

Nughoro amesema wanatarajia idadi ya vifo kuongezeka, na kwamba zaidi ya watu 70,000 wamelazimishwa kuondoka kwenye makaazi yao.

Majeruhi wahamishwa

Baadhi ya majeruhi pia walikuwa wakihamishwa, kwa kuwa hospitali katika mji wa Palu zilikabiliwa na tatizo la ukosefu wa umeme, hii ikiwa ni kulingana na afisa wa jeshi anayehusika na zoezi hilo la kuwahamisha wagonjwa, Bambang Sadewo, aliyesema hawataweza kutibiwa kwenye hospitali hizo.

Taarifa kutoka kituo cha televisheni cha nchini humo cha Metro zimesema kwamba kikosi cha waokozi kimefukua miili 10, iliyofukiwa chini ya kifusi cha hoteli ya ghorofa nane iliyoanguka.Misaada imekwishaanza kuwasilishwa baada ya janga hilo, ingawa kasi imekuwa ndogo kutokana na kuharibika kwa miundombinu.

Mripuko wa Volkano katika mlima wa SoputanPicha: picture-alliance/AP Photo/H. Andih

Rais Joko Widodo, aliyetembelea Palu kwa mara ya pili hii leo, amesema serikali ilikuwa inafanya kila linalowezekana kuwasilisha misaada kwa waathirika wa janga hilo. Amesema, alipokuwa akikagua shughuli za uokozi mahala ilipokuwa hoteli ya Roa Roa, ambako kunaaminiwa bado kuna kuna miili ya watu 60 iliyofunikwa kwamba, misaada ya chakula imeanza kuingia ingawa si kwa kasi kubwa.

Mripuko wa volkano

Katika hatua nyingine, idara ya maafa imeripoti mripuko wa Volkano katika mlima wa Soputan, uliopo eneo jingine kwenye kisiwa hicho cha Sulawesi na moshi uliosabaishwa na mripuko huo uliokwenda kiasi cha kilomita 4 angani.

Hata hivyo hakukua na ripoti za majeruhi na kulingana na Sutopo moshi huo haukuchukuliwa kama kitisho cha kusababisha watu kuhamishwa.

Kitisho cha volkano kimesalia kuwa kidogo lakini wakaazi wana wasiwasi juu ya tishio la matope yanayoweza kutiririka baada ya mripuko.

Mtaalamu wa serikali kwenye masuala ya volkano amesema kuna uwezekano kuwa mripuko huo huenda ukawa umesababishwa na tetemeko hilo la Ijumaa, lililokuwa na ukubwa wa kipimo cha 7.5.

 

Mhariri: Iddi Ssessanga