Uturuki/Syria: Idadi ya watu waliokufa yapindukia elfu 25
11 Februari 2023Mpaka sasa watu wapatao 102,000 wameshahamishwa na kupelekwa sehemu nyingine baada makaazi yao kukumbwa na maafa. Vikosi vya waokoaji karibu 166,000 vinaendelea na juhudi za uokozi ikiwa pamoja na waokoaji kutoka nje.
Mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus pamoja na mratibu wa misaada wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths wamewasili kwenye mji wa Allepo nchini Syria ambako watu zaidi ya milioni 5 wameathiriwa na mitetemeko ya ardhi. Shirika la WHO limepeleka tani 35 za dawa muhimu na msaada mwingine unatarajiwa kupelekwa katika siku mbili zijazo.
Watu kadhaa wameokolewa siku tano baada ya maafa kutokea. Msichana mwenye umri wa miaka 4 alikuwa miongoni mwa waliokolewa kwenye mji wa Gaziantep nchini Uturuki.
Kituo cha radio cha Uturuki kimearifu kwamba mtoto huyo aliokolewa baada ya kuwa chini ya kifusi kwa muda wa saa 130. Shirika la Uturuki linaloshughulikia hali za dharura limesema mitetemeko mingine 1881 ilifuatia nchini Uturuki.
Soma:Shughuli za uokoaji zaendelea Uturuki na Syria huku vifo vikikaribia 25,000
Wakati huo huo vikosi vya uokozi vya Ujerumani na Austria vimesimamisha shughuli za kuwatafuta watu kwenye jimbo la Hatay la nchini Uturuki kutokana na sababu za kiusalama. Pana taarifa juu ya kuzuka mivutano kwenye jimbo hilo na milio ya bunduki ilisikika. Hata hivyo vikosi hivyo vya waokozi kutoka Ujerumani na Austria vitaendelea kuwapo ugani.
Rais Tayyip Erdogan amesema idara husika zilipaswa kufanya haraka ili kuwasaida wahanga. Rais huyo ameahidi kuanza kazi haraka kwa ajili ya ujenzi mpya lakini pia amewaonya wahalifu wanaopora mali za watu wakati huu wa maafa.
Misaada pia imewasili nchini Syria licha ya kuwa ya kiwango cha chini kutokana na athari za vita vya muda mrefu.Shughuli za kupeleka misada hiyo zinatatizika hata baada ya serikali ya nchi hiyo kusema mapema wiki hii kwamba itaruhusu misaada kupelekwa.
Mkuu wa kitengo cha misaada cha Umoja wa Mataifa Martin Griffiths amesifu juhudi zinazofanywa na Uturuki katika kuwashughulikia watu waliokumbwa na maafa ambayo hayajawahi kushuhudiwa katika muda wa karne.
Wakati huo huo mwendesha mashtaka wa serikali nchini Uturuki amesema uchunguzi ufafanywa juu ya majengo yaliyosambaratika ili kubainisha iwapo palikuwapo hitilafu katika ujenzi.
Kwa mujibu wa taarifa, polisi nchini Uturuki wanamshilikia mkandarasi mmoja baada ya kumkamata wakati alipokuwa anasubiri kupanda ndege mjini Istanbul.
Vyanzo:RTRE/AP