1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya watu waliouawa Ghouta Mashariki yafika 40

Caro Robi
7 Aprili 2018

Serikali ya Syria, imeimarisha mashambulizi makali usiku wa kuamkia Jumamosi, katika ngome ya mwisho ya waasi karibu na mji mkuu Damascus nchini Syria, na kusababisha idadi ya raia waliouawa kuongezeka na kufikia 40.

Syrien Syrische Soldaten in Ost-Ghuta
Picha: Imago/Xinhua/A. Safarjalani

Kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za binadamu Syria, mashambulizi hayo pia yameuvunja utulivu ambao umedumu mjini Douma kwa muda wa siku 10 zilizopita.

Mkuu wa shirika linaloangalia haki za binadamu la Syria- Rami Abdel Rahman, ameeleza kuwa mashambulizi hayo ni ya jazba na amezungumzia mamia ya operesheni zilizofanywa Douma.

Abdel Rahman ameongeza kuwa mashambulizi ya makombora kutoka angani yamefanywa sambamba na mashambulizi ya ardhini ambayo yamefanywa na vikosi vya Syria, kusini magharibi na mashariki mwa Douma.

Raia ndiyo waathiriwa wa mapambano

Mwanaharakati Baraa Abdel Rahman ameeleza kuwa hali ya kibinadamu ndani ya Douma ni mbaya sana, majeruhi wengi, wanaaga dunia kufuatia ukosefu wa huduma za afya kwani kuna madaktari wachache waliosalia eneo hilo.

Makombora pia yameanguka katika mji mkuu Damascus na kuwaua takriban watu wanne na kuwajeruhi wengineb 20 katika mitaa ya Barzeh, Al Abaseen na Mazze.

Afisa wa uokozi akimbeba mtoto aliyejeruhiwa mjini DoumaPicha: picture-alliance/AA/M. Abu Taim

Shirika la habari la Syria SANA limeripoti kuwa kundi la waasi la jaish al Islam linahujumu utekelezaji wa makubaliano yaliyosimamiwa na Urusi ya kuruhusu kuondoka kwa wapiganaji wa kundi hilo na familia zao kutoka Douma kuelekea kaskazini mwa Syria na badala yake waasi hao wawaachie huru wafungwa wanaowashikilia.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Syria limesema iwapo makubaliano hayo kati ya Jaish al Islam na Urusi yatafeli ifikapo leo Jumamosi, kuna uwezekano mji wa Douma ukabshuhudia operesheni kubwa ya kijeshi. Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu walioko Douma wamesema mashambulizi yamerejea katika mji huo ili kuwashinikiza wapiganaji waliosalia kuondoka na kuelekea kaskazini mwa Syria.

Siku ya Ijumaa, vikaratasi vilidondoshwa mjini humo vikiwa na ujumbe wa kuwataka waasi kuondoka na kuelekea Jarablus au wasalie Douma na kusalimisha silaha zao ili wapewe msamaha wa serikali. Vijikaratasi hivyo vimewataka raia kusalia na kuwahakikisha usalama wao.

Abdel Rahman amesema waasi wa kundi la Jaish al Islam bado wanakataa kusalimisha silaha zao nzito na wanataka kusalia Douma akiongeza kuna migawanyiko ndai ya kundi hilo kwani baadhi ya wapiganaji wanataka kuondoka , huku wafuasi wa kiongozii wa kidini Abu Abdul Rahman al-Kaaaka wakipinga makubaliano ya kuwataka kuondoka na kutaka kusalia Douma wapigane hadi mwisho.

Katika kipindi cha wiki chache zilizopiza, majeshi ya serikali ya Syria yakisaidiwa na ya Urusi yamefanikiwa kuyakomboa maeneo mengi ya Ghouta Mashariki, eneo ambalo limekuwa mikononi mwa waasi kwa miaka kadhaa sasa.

 

Mwandishi: Caro Robi/dpa/afp

Mhariri: John Juma