Idara za usalama Sudan Kusini ziliwatesa wafungwa.
16 Desemba 2020Kwa mujibu wa shirika hilo, miongoni mwa mbinu za kikatili zinazotumiwa na maafisa wa usalama wa Sudan Kusini ni kuwachoma wafungwa sindano kwenye sehemu za siri, kuwamwagia plastiki iliyochomwa moto kwenye ngozi zao na hata kuwaning'iniza kichwa chini miguu juu kwa muda mrefu.
Na hayo hayaishii hapo. Human Rights Watch inasema kuwa idara hiyo ya usalama wa taifa ya Sudan Kusini inahusika na matukio mengine makubwa ya uhalifu, yakiwemo ya kuwapiga shoti ya umeme watu, ubakaji wa makundi, utekaji nyara na hata mauaji.
Idara hiyo iliyoanzishwa mwaka 2011, muda mfupi baada ya taifa hilo kujitangazia uhuru wake, inafanya kazi nje ya mamlaka yake kikatiba, ambayo ni kukusanya taarifa, kufanya uchambuzi na kuzishauri mamlaka husika, inasema ripoti hiyo iliyozinduliwa mwanzoni mwa wiki hii.
Waandishii wa habari, wanafunzi walilengwa.
Miezi michache tu baada ya kuanzishwa kwake, idara hiyo ilianza kuwafunga jela waandishi wa habari na wakosoaji wa serikali, sambamba na kuchunguza mawasiliano ya simu na ya moja kwa moja, kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyopewa jina: "Ninateswa kwa Uhalifu Gani? Mateso ya Idara ya Usalama wa Taifa ya Sudan Kusini.”
Human Rights Watch inasema chombo hicho sasa kimekuwa miongoni mwa nyenzo kuu za utesaji za serikali, kauli ambayo imekanushwa na kaimu msemaji wa jeshi la Sudan Kusini, Santo Domic Chol, anayedai kuwa shutuma hizo hazina msingi na kwamba hakuna ushahidi kwamba Idara ya Usalama wa Taifa inahusika na matendo ya kikatili kiasi hicho. Kwa mujibu wa kaimu msemaji huyo wa jeshi, "Sudan Kusini ni taifa linaloheshimu sana utawala wa sheria.”
Hata hivyo, ripoti hiyo inasajili matukio kadhaa ambayo mengine yanahusisha muda mfupi baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kuanzia mwezi Disemba 2013, ambapo maafisa wa Idara hiyo walianza msako dhidi ya wakosoaji wa serikali, makhsusi kabisa ikiwalenga watetezi wa haki za binaadamu, wafanyabiashara, waandishi wa habari na wanafunzi.
Wataalamu wa haki za binaadamu wanaitaka serikali kuwashughulikia wahusika.
Ripoti hiyo inatokana na mahojiano na wafungwa wa zamani wapatao 48 na watu wengine 37 wanaojumuisha maafisa wa usalama na familia za watu waliotiwa nguvuni. Utafiti huo ulifanyika baina ya mwaka 2014 hadi 2020, ambapo Human Rights Watch imegunduwa kwamba idara hiyo inafanya kazi bila ya kusimamiwa kisheria sio na mahakama wala na bunge na kwa hivyo maafisa wake wanajiona wana kinga ya kutoshitakiwa.
Idara hiyo inatajwa kuanzisha maeneo yake yenyewe ambayo inayatumia kama mahabusu za wafungwa, ambao huwakamata bila ya kuwa na hati za mahakama. Wengi wa mahabusu hao hushikiliwa kwa miaka kadhaa huku wakiteswa, na hawaruhusiwi kuonana na familia zao wala wanasheria.
Licha ya Sudan Kusini kukana tuhuma zote zinazotajwa kwenye ripoti hiyo, wataalamu wa masuala ya haki za binaadamu wanasema kuwa serikali ina wajibu wa kuchunguza na kuwachukulia hatua wahusika. Phillips Anyang, mwanasheria wa haki za binaadamu kwenye Shirika la Mawakili Wasio na Mipaka, anasema kwamba kiwango cha uhalifu usiochukuliwa hatua unaofanywa na vyombo vya dola kinatisha hasa katika wakati huu ambapo Sudan Kusini inatekeleza makubaliano ya amani kati ya pande hasimu.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AP
Mhariri: Josephat Charo