1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IEBC: Wapiga kura washindwa kusoma na kuandika Marsabit

9 Agosti 2022

Maafisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC katika jimbo la Marsabit wametaja ukosefu wa uwezo wa kusoma na kuandika miongoni mwa wapiga kura kama changamoto kubwa katika eneo hilo.

Kenia Wahlen 2022
Picha: Patrick Meinhardt/AFP

Hali hiyo imechangia zoezi la upigaji kura katika vituo vingi vya kupigia kura katika eneo la Moyale kufanyika taratibu. Shughuli ya upigaji kura katika vituo vingi vya jimbo la Marsabit ilianza kama ilivyokuwa imeratibiwa na IEBC, japo baadhi ya vituo hivyo katika eneo la Loiyangalani vilichelewa kufunguliwa.

Katika eneo bunge la Moyale, hali ya baadhi ya wapiga kura kutokuwa na uwezo wa kusoma na kuandika ilichangia upigaji kura kuendelea polepole kwani maafisa wa IEBC na mawakala wa wagombea walilazimika kuwasaidia wapiga kura hao.

Kila mpiga kura atapata nafasi ya kupiga kura

Lakini, kulingana na msimamizi wa uchaguzi katika eneo la Moyale Jephina Mauta, IEBC itahakikisha kila mpiga kura anapata fursa ya kupiga kura yake licha ya uwezo wake wa kusoma na kuandika.

''Wapiga kura wasiokuwa na uwezo wa kusoma na kuandika wanashauriwa kuja na wasiadizi wao. Iwapo hawatakuwa na uwezo wa kuja na wasaidizi wao, watasaidiwa na maafisa wa uchaguzi kwenye vituo vya kupigia kura mbele ya mawakala,'' alifafanua Mauta.

Afisa wa IEBC akikakua mfumo wa kusimamia uchaguzi Kenya, KIEMSPicha: Brian Ongoro/AFP

Wakati huo huo, mashine tisa za mfumo uratibu wa uchaguzi KIEMS katika eneo la Moyale zilishindwa kufanya kazi na kuilazimu IEBC kuzibadilisha. Mauta amesema kuwa wataongeza muda uliopotezwa kutokana na hitilafu hiyo iliyojitokeza

Mashine zashindwa kufanya kazi

''Kuna visa vya mashine zetu kushindwa kufanya kazi, lakini maafisa wetu wa teknolojia walizibadilisha kwa haraka. Zoezi kwa sasa linaendelea vizuri na hakuna malalamiko zaidi, zile zilikuwepo tumezitatua. Matarajio yetu ni kwamba, kila mpiga kura anapata fursa ya kupiga kura yake,'' alisisitiza Mauta.

Hata hivyo, baadhi ya wapiga kura wamelalamikia kucheleweshwa kwa vifaa vya kupigia kura katika vituo mbalimbali vya Moyale. Shughuli ya upigaji kura katika eneo ya Loiyangalani kwenye eneo bunge la Laisamis lilianza kwa kuchelewa baada ya vifaa vya kupigia kura kutofika kwa wakati stahiki.

Eneo bunge la Moyale lina wapiga kura 68,000 walioandikishwa kushiriki katika uchaguzi mkuu wa Kenya wa Agosti 9, 2022.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW