1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IEBC yatangaza matokeo kutoka maeneo bunge 51 kati ya 290

Babu Abdalla Thelma Mwadzaya
13 Agosti 2022

Tume ya IEBC imetangaza matokeo kutokea maeneo 51 kati ya 290 ya bunge ya uchaguzi wa urais kufikia sasa. Tume hiyo imepewa muda wa hadi tarehe 16 kutangaza matokeo yote.

Kenia Wahlen
Picha: Sayyid Abdul mAzim/AP/picture alliance

Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini Kenya IEBC inaendelea na shughuli ya kujumlisha na kuhakiki matokeo ya uchaguzi kutokea maeneo bunge kwenye ukumbi wa Bomas. Maafisa wasimamizi wa tume wote wameshafika ukumbini kuwasilisha fomu za 34B ili zifanyiwe uhakiki kabla mshindi wa kinyanganyiro cha urais kutangazwa rasmi.

Mapema hii leo, zilizuka sokomoko ukumbini pale wakala wa mgombea wa rais upande wa UDA alipodaiwa kuwa na karatasi zisizoeleweka.Kuhusu tukio hilo Gladys Boss Shollei alikanusha madai na kushikilia kuwa ni utundu wa wapinzani wao, "Karatasi niliyokuwa nayo mkononi ni ratba ya wanaosaidia kuthibitisha fomu zinazofanyiwa uhakiki.Wanajua kabisa hakukuwa na lolote la ajabu. Hata mwakilishi wao anayo karatasi kama hii.Sijaelewa kwanini wamenijia na madai hayo.”

Wakati huohuo, kamishna wa zamani wa tume ya IEBC Roselyn Akombe ameitumia familia ya Daniel Musyoka ujumbe wa pole.

Daniel Musyoka ni afisa msimamizi aliyehudumu kwenye kituo cha Embakasi East cha kuhesabia kura na hajulikani aliko tangu siku ya Alhamisi.Kwa upande wake tume ya IEBC imeweka bayana kuwa imewasiliana na polisi na uchunguzi unaendelea.

Yote hayo yakiendelea,shughuli ya kuhesabu kura kwa kaunti ya Nairobi imeanza tena baada ya kupumzishwa kwa muda mfupi.Shughuli hiyo inafanyika katika uwanja wa michezo wa Kasarani na kufikia sasa matokeo kutokea maeneo 10 kati ya yot 17 yalikuwa yamepokelewa na kuanza kufanyiwa kazi.

Kongamano la kuwatuza washindi

Mgombea mwenza wa muungano wa Azimio la Umoja Martha KaruaPicha: Thomas Mukoya/REUTERS

Kwa upande mwengine, viongozi wa Azimio la Umoja One Kenya wanakutana kwenye jumba la mikutano la kimataifa la KICC kuwatuza waliobuka washindi kwenye uchaguzi mkuu.

Hili ni kongamano la kwanza kufanyika tangu uchaguzi mkuu kupita tarehe 9.Wajumbe hao walishauriwa kuvaa sare za rangi za chama. Mgombea mwenza wa Azimio la Umoja One Kenya Martha Karua anahudhuria kikao hicho pamoja na viongozi wengine.

Wanawake wamejinyakulia ushawishi kwenye uchaguzi mkuu kwani mpaka sasa 7 kati ya wote 47 wamefanikiwa kuwa magavana.

Kaunti ya Nakuru imepata idadi kubwa zaidi ya viongozi wanawake walioshika nyadhifa mbalimbali. Kwa sasa wanawake 7 wamenyakua nafasi za kuwa magavana wa kaunti za Meru, Kirinyaga, Homa Bay, Nakuru na Kwale.

Fatuma Achani ni gavana wa kike wa kwanza kuchaguliwa katika eneo la Pwani na alimshukuru mtangulizi wake,”Tusipelekane mbio nawaomba tudumishe amani.Nataka kumshukuru sana Gavana wa Kwale anayeondoka Salim Mvurya kwa kuniunga mkono na kunipa ushirikiano.Ni mfano mzuri wa kuigwa Kenya nzima kuwa inawezekana kwa gavana kumpigia debe naibu wake na akashinda kwa manufaa ya wakaazi.Mola akubariki sana gavana.”

Nakuru yang'ara kwa kuwachagua wanawake

Picha: Suleiman Mbatiah/AFP

Kwenye orodha ya magavana hao wapya wa kike, 4 ni wa chama cha UDA cha Muungano wa Kenya Kwanza,mmoja wa Wiper na mwenzake wa Orange Democratic Movement-vyama vyote vya Azimio la Umoja One Kenya- na mwengine ni mgombea huru. Kufuataia matokeo hayo, William Ruto wa chama cha UDA aliyepia mgombea wa Kenya Kwanza wa urais amewapongeza viongozi wanawake walioibuka washindi kwenye nyadhifa mbalimbali za kisiasa.Kwenye taarifa yake kupitia mtandao wa Twitter, naibu wa rais William Ruto aliwatakia yote mema wanapojiandaa kutimiza majukumu yao mapya.

Aliwapongeza pia viongozi wote waliojinyakulia nafasi kwenye uchaguzi mkuu.

Jumla ya maeneo bunge 290 yalishirikishwa kwenye uchaguzi mkuu na matokeo yote yanafanyiwa uhakiki kwenye ukumbi wa Bomas of Kenya.Wapiga kura milioni 14 walishiriki kwenye uchaguzi mkuu wa mwanzoni mwa wiki kati ya watu milioni 22 waliosajiliwa.

Siku ya mwisho ya kumtangaza mshindi wa uchaguzi wa rais ni Jumanne.