Ukraine bado yakabiliwa na kizingiti kujiunga na EU
8 Oktoba 2025
Ukraine inatakiwa kuyafanya huku juhudi zikiwa zinaendelea za kuuzima upinzani wa Hungary isiyotaka Ukraine ijiunge na Umoa wa Ulaya.
Ukraine inahitaji kuungwa mkono na nchi zote 27 za Umoja wa Ulaya ili kuwa mwanachama wa jumuiya hiyo lakini Hungary inaizuia kufikia kwenye hatua ya mazungumzo.
Msimamo wa Hungary umeyakatisha tamaa mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya na kamishna anayehusika na upanuzi wa jumuiya hiyo Marta Kos aliuongoza ujumbe wa maafisa wa ngazi ya juu huko nchini Ukraine wiki iliyopita na pia walikutana na jamii ya Wahangari wachache walio magharibi mwa nchi kujaribu kuupunguza mvutano.
Uanachama wa EU ni mwanga wa matumaini kwa Waukraine wengi
Uanachama wa Umoja wa Ulaya ni mwanga wa matumaini kwa raia wengi wa Ukraine kwa siku zijazo ikiwa ni zaidi ya miongo mitatu tangu nchi hiyo ilipopata uhuru wake kutoka kwa Umoja wa Kisovieti.
Mnamo mwaka 2014, rais aliyekuwa anaiunga mkono Urusi Viktor Yanukovych aliondolewa madarakani kufuatia maandamano makubwa baada ya kujaribu kugeuza mwelekeo wa nchi yake katika kutafuta uanachama wa Umoja wa Ulaya.
Vita vya Urusi nchini Ukraine vimeifanya nchi hiyo kuvutiwa zaidi na hatua za kujiunga na Umoja wa Ulaya, zaidi kwa raia wa Ukraine wanaopendelea kuwa karibu na nchi za magharibi.
Lakini kutokana na hatua ya Kyiv katika kipindi cha majira ya joto ya kujaribu kuubana uhuru wa waangalizi ilizitishia serikali nyingi za Ulaya na kuzua changamoto za mageuzi zinazoikabili Ukraine ambayo inahitaji kurekebisha sheria zake ili zikidhi viwango vya Umoja wa Ulaya.
Kwa sheria za Umoja wa Ulaya jumuiya hiyo haiwezi kuikubali nchi kuwa mwanachama mpya kama haikidhi viwango vya utawala wa sheria kwa asilimia 100.
Kizuizi cha Hungary
Kamishna anayehusika na upanuzi wa kanda ya Umoja wa Ulaya, Marta Kos amesema licha ya wanachama wa Umoja wa Ulaya kuipenda Ukraine lakini linapokuja suala la mageuzi katika maeneo yote kuanzia kwenye kilimo hadi mazingira hapo ndio Ukaine inayotaka kujiunga na umoja huo itakabiliwa na kazi ngumu.
Kos amesema bila mageuzi Ukraine itajikuta mahala pagumu katika azma yake ya kujiunga na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya
Naibu Waziri Mkuu wa Ukraine Taras Kachka ambaye pia anahusika na Ushirikiano wa wa nchi yake na Ulaya amesema Ukraine inachukua kila hatua na mbinu za kivitendo na itaendelea kufanya mageuzi ili kuweza kusonga mbele haraka inavyowezekana kuingia kwenye hatua inayofuata ya mchakato wa kujiunga na Umoja wa Ulaya.
Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban mnamo mwaka 2023, alichagua kutopinga uamuzi wa viongozi wa Umoja wa Ulaya wa kufungua mazungumzo ya Ukraine kujiunga na Umoja wa Ulaya lakini sasa Hungary inaizuia Ukraine kusonga mbele kwenda kwenye hatua inayofuata ya mazungumzo juu ya vipengee katika mada zinazohusu sera mbalimbali.
Rais wa Halmashauri ya Ulaya Ursula von der Leyen amesema Ukraine inaweza kujiunga na kambi ya Umoja wa Ulaya kabla ya mwaka 2030 ikiwa itaendelea na mageuzi kwa kasi na ubora lakini muda huo unatiliwa mashaka na baadhi ya wahusika.