1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Ikulu ya Kremlin yakataa kuthibitisha mazungumzo na Marekani

7 Novemba 2022

Ikulu ya Urusi Kremlin, imekataa kutoa maoni kuhusu ripoti ya jarida la Wall Street kwamba Marekani ilifanya mazungumzo ya faragha na maafisa wakuu wa nchi hiyo kuhusu kuepusha kuongezeka kwa vita nchini Ukraine.

Russland Dmitri Peskow Kremlin Sprecher
Picha: Sefa Karacan/AA/picture alliance

 

Kulingana na ripoti hiyo, mshauri wa usalama wa kitaifa wa Marekani Jake Sullivan, alifanya mazungumzo na wasaidizi wa rais Vladimir Putin kwa matumaini ya kupunguza athari zinatokana na vita nchini Ukraine ama kuongezeka kwa vita hivyo kuwa mzozo wa nyuklia. Msemaji wa ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov, amesema hawana la kusema kuhusu chapisho hilo. Peskov ameendelea kusema kuwa anarudia kwa mara nyingine tena kwamba kuna ripoti za ukweli lakini kwa kiasi kikubwa , kuna ripoti ambazo ni uvumi mtupu.

Marekani yasisitiza mazungumzo ya kumaliza vita ni kati ya Urusi na Ukraine

Katika miezi ya hivi karibuni, mawasiliano machache ya kiwango cha juu kati ya maafisa wa Marekani na Urusi yametangazwa hadharani huku Marekani ikisisitiza kuwa mazungumzo yoyote ya kumaliza vita nchini Ukraine yatafanywa kati ya Urusi na Ukraine.

Huku hayo yakijiri, Ukraine imesema silaha iliyopokea Jumatatu (7.11.2022) zitasaidia kujilinda dhidi ya mashambulizi ya Urusi ambayo hivi karibuni yalilenga miundombinu ya nishati. Kupitia ujumbe katika mitandao ya kijamii, waziri wa ulinzi wa Ukraine Olkeksiy Reznikov, amesema mifumo ya ulinzi wa anga ya NASAMS na Aspide tayari imewasili Ukraine na kwamba silaha hizo zitaimarisha kwa kiasi kikubwa jeshi la Ukraine na kufanya anga yao kuwa salama zaidi.

Majengo yalioharibiwa kwa mashambulizi Kherson nchini UkrainePicha: Metin Aktas/AA/picture alliance

Reznikov ameongeza kwamba wataendelea kulenga maeneo ya maadui wanaowalenga na kuwashukuru washirika wao Norway, Uhispania na Marekani. Reznikov pia amesema kuwa mwezi uliopita, Ukraine ilipokea mfumo wake wa kwanza wa ulinzi wa Iris-T kutoka Ujerumani.

Mbali na hayo,  mamlaka ya Kyiv imesema kuwa hali inayozunguka uwezo wa mji huo kusambaza nishati kwa wakazi bado ni ya wasiwasi na imewahimiza raia katika mji huo mkuu kupunguza matumizi ya umeme. Kupitia mtandao wa Telegram, mamlaka hiyo imewataka wakazi wa eneo hilo kuwasaidia wafanyakazi katika sekta hiyo ya nishati wanaopambana kusawazisha hali hiyo. Mashambulizi ya Urusi katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita yameharibu karibu theluthi moja ya vituo vya umeme vya Ukraine na serikali ya Ukraine imewataka raia wake kubana matumizi ya nishati ya umeme kadri wawezavyo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW