Ikulu ya White House yakosoa matamshi ya Trump dhidi ya NATO
11 Februari 2024Siku ya Jumamosi, Trump alisema aliwahi kumweleza kiongozi wa taifa moja mwanachama wa NATO kuwa Marekani haitotoa ulinzi kwa mataifa yasiyotimiza wajibu wake wa kulipia kiwango cha bajeti cha kuendesha mfungamano huo wa kijeshi.
Soma pia:Trump aziwashia moto nchi za NATO
Vilevile amesema alieleza bila kificho kwamba iwapo shambulio litatokea, atawahimiza wavamizi "kufanya wanavyotaka".
Matamshi hayo ya Trump yamezusha ukosoaji mkubwa kutoka kwa wanasiasa nchini Marekani.
Msemaji wa White house asema kuhimizia uvamizi kutahatarisha usalama wa Marekani
Akizungumzia matamshi hayo ya Trump, msemaji wa ikulu ya White House Andrew Bates, alisema kuhimiza uvamizi wa washirika wao wa karibu kutoka kwa kile alichokiita ''tawala za mauaji'' kunahatarisha usalama wa taifa wa Marekani, utulivu wa kimataifa na uchumi wa nchi hiyo.
Soma pia:Katibu Mkuu wa NATO kukutana na Donald Trump
Kupitia taarifa aliyotoa jana jioni, Bates ameongeza kuwa badala ya kuitisha vita na kuendeleza machafuko, Rais wa nchi hiyo Joe Biden ataendelea kuimarisha uongozi wa Marekani na kusimamia maslahi ya usalama wa kitaifa.