ILO: Mizozo yachangia kudorora kwa soko la ajira duniani
31 Oktoba 2022Ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la ILO imetahadharisha kuwa mwelekeo wa soko la ajira ulimwenguni umepungua katika miezi ya hivi karibuni, wakati ambapo vita vya Ukraine na mizozo mingine inayoingiliana ikisababisha kupungua kwa mishahara, madeni makubwa na kukosekana kwa usawa.
Mkurugenzi Mkuu mpya wa ILO, Gilbert Houngbo, amewaambia leo waandishi habari kwamba shirika hilo linakadiria kuwa iwapo mwenendo wa sasa utaendelea, ukuaji wa ajira duniani utashuka kwa kiasi kikubwa katika miezi mitatu ya mwisho wa mwaka huu wa 2022 na ukosefu wa ajira unaweza kuongezeka.
Serikali ziweke sera za kina
Houngbo amezitolea wito serikali kuingilia kati kusaidia kupanga bei za bidhaa, na kuendelea kusaidia katika mapato na ulinzi wa kijamii, kwa kuwepo mazungumzo ya kina ya kijamii ili kuunda sera zinazohitajika kukabiliana na kushuka kwa soko la ajira. Amesema ili kukabiliana na hali hii ya ajira duniani inayotia wasiwasi sana na kuzuia kudodora kwa soko la ajira, panahitajika sera za kina, zenye uwiano kitaifa na kimataifa.
Mkurugenzi huyo wa Shirika la Kazi Duniani, amesema kumalizika haraka kwa vita vya Ukraine, kutazidi kuchangia katika kuimarisha hali ya ajira ulimwenguni.
ILO pia imebaini kuongezeka kwa muda wa saa za kazi duniani mwanzoni mwa mwaka huu, hasa miongoni mwa wanawake na wanaofanya kazi za ustadi wa hali ya juu, wakati ambapo uchumi wa dunia unaanza kuimarika kutokana na athari za wakati wa janga la virusi vya corona. Hata hivyo, kaya nyingi bado zinakabiliana na kushuka kwa mapato kutokana na janga la COVID-19.
Shirika hilo ambalo limechapisha toleo la 10 la ripoti yake ya kufuatilia ajira ulimwenguni, limesema hali imezorota huku idadi ya saa za kazi ikipungua kwa asilimia 1.5, sawa na upungufu wa ajira za kutwa zipatazo milioni 40, ambapo watu hufanya kazi kwa muda wa saa nane kwa siku.
Soko la ajira halina uhakika kwa sasa
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mwonekano wa soko la ajira kwa sasa hauna uhakika sana, huku kukiwa na hatari zinazoongezeka ikiwemo athari za mfumuko mkubwa wa bei, sera za kubana matumizi ya fedha, kuongezeka kwa mzigo wa madeni na kupungua kwa imani ya walaji.
Ingawa huchukua muda kwa uchumi ulioshuka au kudorora kwa uchumi, kusababisha uharibifu wa kazi na ukosefu wa ajira, takwimu zilizopo zinaonesha kuwa tayari soko la ajira kwa wafanyakazi linapungua kwa kasi. ILO inakadiria kuwa zaidi ya asilimia 10 ya wafanyakazi wa kabla ya vita vya Ukraine, wengi wao wakiwa wanawake, kwa sasa wako katika nchi jirani kama wakimbizi.
Mfumuko wa bei katika nchi hiyo iliyoharibiwa na vita, unatarajiwa kuwa juu kwa asilimia 30 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, huku ILO ikikaridia kuwa ajira zitakuwa asilimia 15.5 chini ya viwango vya mwaka 2021.
(AP, AFP, DPA, Reuters)