Ilwad Elman, Mshindi wa Tuzo ya Ujerumani kwa Afrika
20 Oktoba 2020Ilwad ana umri wa miaka 30, lakini anachukuliwa kuwa miongoni mwa watu muhimu wenye ushawishi Somalia wakati nchi hiyo kwa sasa ikielekea kuwa na uthabiti.
Jitihada zake zimesababisha wakfu wa Ujerumani na Afrika kutoa tuzo yake mashuhuri kwa mwanadada huyo mtaalamu anayetambuliwa kimataifa kwa utatuzi wa mizozo, aliyechaguliwa kutoka kwa orodha ya wagombea 30.
Wakati Somalia ilipoingia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe mwanzoni mwa miaka ya 1990, baba yake Elman Ali Ahmed mhandisi, mjasiriamali na mwanaharakati wa kijamii alikuwa ameanzisha mipango ya kuwasaidia kuwapa ujuzi na kuwarekebisha tabia watoto waliokuwa wanajeshi na yatima wa vita nchini Somalia.
Wakati hali ya usalama ilipovurugika na kuwa mbaya mjini Mogadishu, Ilwad na mamake walilazimika kukimbilia Canada akiwa na umri wa miaka miwili, huku babake akibakia Somalia lakini aliuawa mnamo 1996.
Migogoro ya silaha
Licha ya hatari iliyokuwepo, Ilwad alirudi Somalia mnamo 2010 pamoja na mamake na dada zake kuendelea na kazi ya baba yake. Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, Ilwad na mama yake, Farttun Adan, wameunda Kituo cha Amani cha Elman, na kupitia shirika hilo lisilo la kiserikali lenye wafanyikazi 172 na matawi manane ya mkoa.
Awali Ilwad alipata nafasi ya kushiriki katika maadhimisho ya 12 ya wadau kuhusu jukumu la watoto na migogoro na silaha alisema,"ingawa imekuwa miaka 20 tangu baba yangu auawe kwa kazi hii, kazi ya kuwapokonya silaha na kuwashauri watoto inaendelea Somalia bado ni muhimu sana hadi leo huko Somalia, na mkutano huu usio rasmi unaleta tija ulimwenguni kote."
Pamoja na mama yake, Ilwad Elman alichukua mradi wa baba yake wa kuwaunganisha watoto wanajeshi na watoto yatima wa vita vya wenyewe kwa wenyewe katika jamii ya Somalia. Kupitia mpango wake ulioheshimiwa sana wa elimu wenye kauli mbiu "Dondosha bunduki, chukua kalamu" amesaidia maelfu ya vijana kuzowea maisha ya uraia.
Mpango huo umefanikiwa, kutokana na njia zake za kisasa za matibabu, mipango ya mafunzo bila malipo na mipango ya ubunifu ya kifedha, sasa imeanza kutumika Mali na eneo la Ziwa Chad.
"Nina furaha kubwa kupokea utambuzi huu kutoka Ujerumani," Ilwad aliiambia DW baada ya kusikia taarifa kuhusu tuzo yake.
"Tuzo ni pongezi kubwa kwa Timu yetu na ni muhimu kwa sababu Ujerumani ni mshirika muhimu na wa kuaminika katika miradi yetu mingi, " asema Ilwad Elman.