Imani Imesalitiwa – Hadithi ya Udhalilishaji wa Kijinsia Barani Afrika
6 Agosti 2013Kila mara mtu anaponyanyaswa kimapenzi au kubakwa, huwa amedhulumiwa. Dhulma ya aina hii mara nyingi hufanyika kwa usiri mkubwa na wanaodhulumiwa huogopa au wanaona aibu kujitokeza hadharani.
Katika mchezo huu wa “Usaliti wa Imani”, tunafuatilia hadithi ya Pato, Nuru na Allan, ambao wamedhulumiwa kimapenzi kwa namna moja au nyingine. Pato, mwanafunzi mwenye umri wa miaka 16, anajaribu kuficha siri kuhusu tabia ya mwalimu anayemtaka kimapenzi. Lakini anaposhindwa kuvumilia anafichua siri hiyo kwa rafiki zake.
Na katika sehemu nyingine ya nchi hiyo, mashambulizi ya waasi ni jambo la kawaida. Tunakutanna na Nuru, mwanamke mwenye umri wa miaka 30, ambaye anaishi na makovu baada ya kubakwa na waasi. Aidha kisa hicho kimeyaathiri maisha yake ya ndoa, kwani mumewe anajihisi mdhaifu na mwenye machungu kuweza kustahimili kisa alichotendewa mkewe.
Kwa upande mwingine kijana Alan mwenye umri wa miaka 10 anashindwa kuvumilia na kujitokeza hadharani kumueleza mama yake kuhusu ukatili unaotekelezwa na baba yake wa kambo. Maisha ya vijana hawa watatu ni ya kusikitisha.
Lakini wanafahamu kwamba wanaweza kupata msaada ili kujikwamua kutoka maisha haya. Mwanamke mmoja jasiri kwa jina Judy, amezindua shirika la kupambana na dhulma za aina hii “Pambana na Unyanyasaji wa Kimapenzi” na linakubali kuwasaidia waathiriwa kama Pato, Nuru na Allan.
Sikiliza mchezo huu “Imani Imesalitiwa”,ufahamu jinsi vijana hawa watatu walivyojinusuru baada ya visa hivi vya dhuluma.
Noa Bongo Jenga Maisha Yako ni vipindi vinavyotayarishwa na Deutsche Welle na vinasikika katika lugha sita ikiwa ni pamoja na Kiingereza, Kiswahili, Kifaransa, Kihausa, Kireno na Kiamhara.