Imekuwa vigumu kuwapeleka watoto shuleni nchini Zimbabwe
28 Januari 2008Alois Mufundisi, mfanyakazi katika vyombo vya habari hupata mshahara wa dola milioni mbili za Zimbabwe, ambazo ni kiasi cha dola 50 za kimarekani. Kiwango hiki ni kikubwa kwa kukitazama lakini katika hali halisi ya kimaisha kinatosha tu kununua chakula kwa muda wa nusu mwezi.
Pesa hazimtoshi kumuwezesha kuwalipia karo ya shule watoto wake watatu. Miaka saba iliyopita aliweza kuishi bila matatizo lakini sasa analazimika kufanya kazi za ziada kuongeza mapato yake. Nchini Zimbabwe imekuwa vigumu kuwapeleka watoto shuleni.
´Mara nyingine siwezi kulala nikifikiria ni wapi nitakakopata dola nyengine. Inaniuma kufikira kwamba huenda nisiweze kugharimia vitu vya msingi kama vile elimu ya watoto wangu,´amesema Mufundisi.
Huku mfumuko wa bei ukikadiriwa kuwa asilimia 8000, imekuwa vigumu kuhakikisha watoto wanaelendelea na masomo yao shuleni. Viwango vya elimu vimekuwa vikishuka kwa kasi kubwa tangu kuporomoka kwa uchumi mnamo mwaka wa 2000, wakati maelfu ya mashamba yaliyokuwa yakimilikiwa na wazungu yaliponyakuliwa na serikali.
´Wakati wetu elimu ilikuwa bure, ´amesema Mfundisi. Wazazi wake wangempeleka pamoja na ndugu zake kusoma katika shule za bweni kutumia mshahara wa babake aliyekuwa akifanya kazi na serikali. Lakini sasa anakabiliwa na kitisho cha kutoweza kuwapeleka watoto wake shuleni.
Shule zilifunguliwa nchini Zimbabwe mnamo tarehe 15 Januari na walimu katika shule za mjini Harare wameripoti idadi kubwa ya wanafunzi wanaokosa kwenda shule ikiendelea kuongezeka kila kuchao. Hali inazidi kufanywa kuwa ngumu kutokana na ukosefu wa chakula, pesa na mafuta huku Zimbabwe ikikabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi.
Mfumo wa elimu nchini Zimbabwe ambao ulikuwa miongoni mwa mifumo bora ya elimu barani Afrika, umetumbukia katika mzozo mkubwa. Maelfu ya walimu katika shule za serikali mara kwa mara wanafanya mgomo baridi wakidai nyongeza ya mishahara. Walimu wengi wanakimbia Zimbabwe kwenda kufanya kazi zenye mishahara minono katika nchi jirani.
Chama cha walimu cha Zimbabwe, Progressive Teachers Union of Zimbabwe, kinakadiria walimu zaidi ya 15,000 waliacha kazi mnamo mwaka wa 2006. Wale wanaobakia hutumia wakati wao mwingi wakijitafutia pesa zaidi. Hata walimu wakuu katika shule za kibinasfi, ambako elimu ni ya kiwango cha juu, wanadai rushwa hadi randi 200 za Afrika Kusini ama dola 50 za kimarekani, kuwasajili wanafunzi wapya.
Alois Mfundisi ameliambia shirika la habari la IPS kwamba alilazimika kulipa pesa za kigeni ili apate nafasi ya mtoto wake wa kike katika shule moja ya kibinafsi mjini Harare. Mwalimu mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe ameliambia shirika hilo la habari kwamba anaacha kazi yake ya ualimu na kwenda Afrika Kusini. Ameuza vitabu vya maktaba ya idara yake kuongezea mshahara wake mdogo. ´Nalazimika kukimbia kabla sijakamatwa,´ ameongeza kusema mwalimu huyo.
Uwekezaji katika elimu uliofanywa na rais Robert Mugabe tangu uhuru wa Zimbabwe mnamo mwaka wa 1980, umeonekana kama nguzo ya utawala wake wa kiimla wa miaka 27, ingawa alirithi miundombinu mingi kutoka kwa serikali ya ukoloni. Chama wa walimu cha Zimbabwe kinakadiria kati ya wanafunzi wanne hadi watano wanalazimika kutumia kitabu kimoja. Wanafunzi wanne wanatumia dawati moja katika madarasa ambayo yako katika hali mbaya.
Wanafunzi wanazimia madarasani kutokana na njaa. Wasichana hawaendi shule wakati wa siku za hedhi kwa sababu hawawezi kununua pedi. Kasi ya wanafunzi kuacha kwenda shule inazidi kuongezeka. Wanafunzi wanaacha masomo ili kutafuta kazi kama wachuuzi, kondakta wa kukusanya nauli katika mabasi na hata makahaba.
Sheria ya kudhibiti bei za vyakula iliyotangazwa mwezi Juni mwaka jana ilisababisha bidhaa zote kupotea madukani. Lakini sheria hii iliondolewa kwa awamu ili kurejesha thamani kwa watengenezaji bidhaa na biashara. Hata hivyo haijakuwa rahisi kupata chakula. Baadhi ya shule za bweni zinazokabiliwa na ukosefu wa chakula zimesisitiza wanafunzi wajibebee chakula kutoka nyumbani.
Elimu ya juu pia inakabaliwa na matatizo. Chama cha kitaifa cha wanafunzi wa vyuo vikuu, ZINASU, kilitoa ripoti yake wiki iliyopita iliyosema Zimbabwe ina kiwango kikubwa cha wanafunzi wanaoacha masomo ya juu nje ya eneo linalokabiliwa na vita. Ripoti hiyo inasema zaidi ya asilimia 31.5 ya wanafunzi waliacha masomo kwa sababu ya karo nyingi wanazotakiwa kulipa katika taasisi hizo.
Ripoti hiyo pia ilisema Zimbabwe inakabiliwa na upungufu wa bajeti ya elimu ya juu, kuzorota kwa kazi ya ualimu, kuharibika kwa vifaa vya elimu na miundombinu, migomo ya wanafunzi, kuvurugika kwa elimu ya vyuo vikuu, upungufu wa walimu wenye ujuzi na waliopokea mafunzo ya ualimu, ukosefu wa uhuru wa elimu na ongezeko la ukosefu wa kazi miongoni mwa wanafunzi wa vyuo vikuu wanaomaliza masomo yao.