1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IMF kupunguza makadirio ya ukuaji uchumi

Josephat Charo
13 Mei 2020

Mkuu wa shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, Kristalina Georgieva, amesema kuna uwezekano mkubwa shirika hilo likapunguza makadiro yake ya ukuaji wa uchumi wa dunia.

Kristalina Georgieva
Picha: Reuters/R. Casilli

Akizungumza katika mkutano kwa njia ya video ulioandaliwa na gazeti la Financial Times, Georgieva amesema data wanazozipokea kutoka nchi nyingi ni mbaya kuliko ilivyokadiriwa awali na kwamba wanatarajia kupata habari mbaya zaidi mwaka huu.

Shirika la IMF mwezi uliopita lilikadiria kwamba kufungwa kwa biashara na hatua kali za kufunga shughuli nyingi za kila siku kote duniani kungeutumbukiza ulimwengu kwenye mgogoro mkubwa wa kiuchumi tangu mdororo mkubwa kabisa wa uchumi wa miaka ya 1930, huku pato jumla la ndani likinywea kwa asilimia tatu mwaka huu.

IMF na Benki ya Dunia zatakiwa kufuta madeni ya nchi masikini

Kauli ya Georgieva inakuja wakati wabunge zaidi ya 300 kutoka maeneo mbali mbali ya ulimwengu wakilitaka shirika la IMF na benki ya dunia kufuta madeni ya nchi masikini kabisa, kama hatua ya kuzisaidia kupambana na janga la virusi vya corona.

Mpango huo unaoongozwa na mgombea uraisi wa zamani wa Marekani, seneta Bernie Sanders na mbunge Ilham Omar wa chama cha Democratic kutoka jimbo la Minnesota, unakuja wakati kukiwa na wasiwasi kwamba nchi zinazoendelea na zinazoinukia kiuchumi zitaathiriwa na kuvurugwa vibaya na janga hilo.

Bernie Sanders, mgombra urais wa zamani wa MarekaniPicha: Reuters/L. Jackson

Shirika la IMF tayari limeidhinisha msaada wa fedha kwa nchi 50 wanachama wakati huu wa janga la COVID-19. Akizungumza mjini Washington, msemaji wa IMF, Jerry Rice, amesema shirika hilo linataka kusitisha ulipaji wa madeni kwa nchi masikini kabisa duniani.

"Shirika la IMF kwa upande kupitia idhini ya bodi ya utendaji, limeendelea na mpango wa utoaji wa fedha za msaada kwa nchi 25 kutoka kwa hazina ya kushughulikia majanga na utoaji wa misaada. Hii inazisaidia nchi masikini kabisa kutenga fedha zaidi kwa ajili ya utoaji wa huduma muhimu za afya zinazohitajika sana, badala ya kulipa madeni yanayotakiwa kulipwa kwa IMF."

Kenya yaonywa kuhusu mzigo wa madeni

Wakati huo huo shirika la IMF limepandisha kiwango cha kitisho cha Kenya kulemewa na madeni yake kutoka kima cha wastani hadi cha juu kwa sababu ya janga la corona. Deni la taifa hilo la Afrika Mashariki lilikuwa ni asilimia 61.7 ya pato jumla la taifa kufikia mwishoni mwa mwaka uliopita, kutoka asilimia 50.2 mwishoni mwa mwaka wa 2015, hali ambayo IMF inasema ilisababishwa na miradi mikubwa ya ujenzi wa miundombinu, kama vile reli mpya ya kisasa.

Kwa upande mwingine, Misri imepokea dola bilioni 2.77 kama msaada wa dharura wa fedha kutoka kwa IMF kuisadia kudhibiti janga la ugonjwa wa COVID-19 ambalo limeikwamisha kabisa sekta yake ya utalii na kusababisha uhamishaji wa mitaji nje ya nchi.

Shirika la IMF pia limesema jana kwamba mkurugenzi wake atapendekeza kuidhinisha ombi la Chile la mkopo wa dola bilioni 23.8 kulisaidia taifa hilo la Amerika Kusini, linaloongoza duniani kwa uzalishaji wa shaba, huku likikabiliana na changamoto chungu nzima kutokana na janga la corona na kuporomoka vibaya sana kwa bei za bidhaa.

(rtre,afp)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW