1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiChina

IMF yatabiri ukuaji uchumi wa dunia kwa mwaka 2023

31 Januari 2023

Shirika la Fedha la kimataifa, IMF limesema ukuaji uchumi wa dunia unatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 2.9 mwaka huu na kuongeza utabiri wake kuhusu matumizi makubwa ya kushangaza na uwekezaji

IWF Direktorin Kristalina Georgieva
Picha: Britta Pedersen/dpa/picture alliance

Uchumi wa dunia umeathirika kutokana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, kuzorota kwa uchumi na jitihada za kukabiliana na kuongezeka kwa gharama za maisha.  Kutokana na hali hii, Shirika la IMF linatarajia uchumi wa dunia kutanuka kwa asilimia 2.9  mwaka huu, hiki kikiwa kiwango kilichopungua kutoka mwaka 2022 hadi kiwango ambacho bado ni dhaifu kulingana na viwango vya kihistoria. Katika ripoti yake ya hivi karibuni ya Mtazamo wa Kiuchumi Duniani, IMF imesema kwamba hatari mbaya zimethibitiwa tangu ubashiri wa mwezi Oktoba mwaka jana.

Mwaka huu bado wakadiriwa kuwa na changamoto

Mchumi Mkuu wa shirika la IMF, Pierre-Olivier Gourinchas, amewaambia waandishi habari kwamba mwaka huu bado utakuwa na changamoto, lakini huenda kutakuwa na mabadiliko ya ukuaji wa uchumi na kupungua kwa mfumuko wa bei. Shirika hilo hasa, limesema kuwa linaziona Ujerumani na Italia zikiepukana na mdororo wa uchumi, tofauti na utabiri wa awali wakati ambapo uchumi wa Ulaya umeonesha ustahimilivu kuliko ilivyotarajiwa, licha ya vita vya Ukraine.

Pierre-Olivier Gourinchas - Mchumi mkuu wa IMFPicha: Patrick Semansky/AP/picture alliance

IMF pia imesema kwamba utabiri wa ukuaji mdogo wa uchumi mwaka 2023, unaonesha kupanda kwa viwango vya benki kuu kukabiliana na mfumuko wa bei hasa katika nchi zilizoendelea kiuchumi pamoja na vita nchini Ukraine. Lakini ijapokuwa uchumi wa Marekani unakadiriwa kushuka hadi asilimia 1.4 mwaka huu, na eneo linalotumia sarafu ya Euro likitarajiwa kushuka hadi asilimia 0.7, takwimu zote mbili zinaonyesha ukadiriaji wa ongezeko kutoka mwezi Oktoba mwaka uliopita.

Uchumi ulionesha ustahimilivu wa kushangaza kutoka robo ya tatu ya mwaka uliopita

Gourinchas amesema ukuaji wa uchumi ulionesha ustahimilivu wa kushangaza kutoka robo ya tatu ya mwaka uliopita kwa kuwa na masoko thabiti ya kazi, matumizi makubwa ya nyumba na uwekezaji wa biashara. Gourinchas ameongeza kuwa mataifa pia yalishughulikia vizuri kuliko ilivyotarajiwa mzozo wa nishati barani Ulaya na kushuhudia bei ya gesi ya chini kuliko ilivyotarajiwa na kuwa na raslimali za kutosha kuhakikisha kuwa hakuna uwezekano wa uhaba wa bidhaa hiyo katika msimu huu wa baridi.

Mchumi huyo pia amesema kuwa mfumuko wa bei umeonesha dalili za kushuka kote duniani huku hatua ya kufunguka tena kwa China ikileta matumaini ya kufufuka kwa haraka kwa shughuli za kiuchumi nchini humo. Awali, mkuu wa IMF Kristalina Georgieva, alisema kuwa katika siku za nyuma, taifa hilo lenye uchumi wa pili mkubwa zaidi duniani lilichangia hadi aslimia 40 ya ukuaji wa uchumi wa dunia.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW