1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi zinazoendelea kukabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi

17 Machi 2020

Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan anahofu kuwa virusi vya Corona vitaathiri uchumi wa nchi zinazoendelea na kuzionya nchi tajiri kuwa tayari kulipa madeni ya nchi maskini duniani.

Screenshot Exklusivinterview mit Imran Khan
Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan

Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan ni kiongozi ambaye hachelei kuwa muwazi.

Katika mahojiano na shirika la habari la Associated Press, Khan ametoa wito kwa mataifa tajiri kuzitazama kwa jicho la huruma nchi maskini na hata kuzilipia madeni yao wakati huu ambapo virusi vya Corona vinaendelea kuenea kwa kasi katika mataifa mbalimbali duniani.

Khan amesema kuwa iwapo kutatokea mlipuko wa COVID-19 nchini Pakistan, ana wasiwasi kuwa uchumi wa nchi hiyo utaporomoka kwa kiwango cha kutisha. Nchi hiyo ilioko kusini mwa bara Asia, ilichukua mkopo wa dola bilioni 6 za kimarekani mwaka uliopita kutoka shirika la fedha duniani(IMF). Khan amesema "Kwa sababu ya athari ya kuporomoka kwa uchumi, wasiwasi wangu ni umaskini na njaa. Hali hiyo inanitia hofu zaidi. Nadhani jamii ya kimataifa inafaa kufikiria kuondoa madeni kwa nchi maskani kama sisi ambazo huenda zikaathirika zaidi. Angalau hiyo itatusaidia."

Hadi sasa, Pakistan imethibitisha kesi 183 za maambukizi  ya virusi vya Corona.

Vile vile, Khan ameitaka Marekani iondoe vikwazo vilivyoiwekea Iran ambayo imekuwa kiini cha mlipuko wa virusi vya Corona katika eneo la Mashariki ya Kati.

Wanafunzi wa Pakistan wakivaa vifaa vya kuziba pua kujikinda dhidi ya virusiPicha: Getty Images/AFP/A. Qureshi

Kiongozi huyo ameongeza kuwa kando na Pakistan, India na nchi za Afrika zitaathirika zaidi na virusi hivyo kutokana na ukosefu wa raslimali na vifaa vya kisasa.

Janga la virusi vya Corona linachukuliwa kuwa mtihani mkubwa kwa utawala wa Khan tangu alipochukua hatamu za uongozi mnamo mwaka 2018. Waziri Mkuu huyo amepata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa vijana.

Hata hivyo, wakosoaji wake wanahoji kuwa Khan aliingia mamlakani kwa kutumia nguvu za kijeshi huku nayo makundi ya kutetea haki za kibinadamu yakisema utawala wake umebinya uhuru wa vyombo vya habari hasa vile ambavyo vimekuwa vikikosoa utawala wake.

Watu wengi ambao wameambukizwa virusi vya Corona wamekuwa wakipata homa na kukohoa lakini huenda pia wakapata hali ya matatizo ya kupumua. Virusi hivyo vimeathiri zaidi wazee na watu wenye kinga dhaifu dhidi ya magonjwa.

 

Vyanzo AP