1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Imran kumwita Osama shahid ni kuteleza ulimi?

26 Juni 2020

Waziri mkuu wa Pakistan Imran Khan amezusha utata mkubwa kwa kumuita aliyekuwa kiongozi wa mtandao wa harakati za ugaidi duniani wa al-qaida,Osama Bin Laden kuwa ''Shahid''.

Osama Bin Laden Porträt
Picha: Getty Images/AFP

Mwandishi wa DW Shamil Shams ameandika uhariri ufuatao akisema, anaamini tamko hilo la waziri mkuu Khan linaambatana na mtazamo wake wa kibinafsi na kisiasa. Sio siri kwamba waziri mkuu wa Pakistan Imran Khan anahisia za kuegemea upande wa wanaitikadi kali hata kwa wale wanamgambo wanaofanya mashambulizi nchini Afghanistan na Pakistan.

Anailaumu Marekani kwa kuivuruga hali ya usalama wa eneo la Afghanistan na Pakistan na kuhalalisha harakati za wanamgambo wakitaliban kama ni matukio ya athari zinazotokana na uvamizi wa nchi yenye nguvu. Lakini kumuita aliyekuwa kiongozi wa mtandao wa kigaidi wa alqaeda,Osama Bin Laden kuwa ni Shahid ni kiwango kingine kabisa cha kuvuka mpaka hata kwake mwenyewe Khan.

Baadhi ya watu wanasema aliteleza ulimi. Lakini mwandishi wa DW aliyeandika uhariri huu anasema yeye analiona lilikuwa ni kosa ambalo waziri mkuu huyo hakukusudia kulifanya na ambalo limefichua hisia za fikra zake. Mnamo Juni 25 katika hotuba yake bungeni waziri mkuu Khan alitakiwa kuumaliza wasiwasi wa upinzani kwamba serikali yake imeusimamia vibaya mgogoro wa virusi vya Corona nchini Pakistan,lakini hakufanya hivyo badala yake aliamua kuliweka pembeni suala hilo na kuzungumzia kwa kirefu kuhusu masuala mengine mengi ikiwemo vita dhidi ya ugaidi na jinsi vilivyoiharibu Pakistan.

Huu ndio mwelekeo wa Imran Khan?

Waziri Mkuu wa Pakistan Imran KhanPicha: Getty Images/AFP/A. Qureshi

Huu lakini ndio mwelekeo wake wa kisiasa aliokuwa akiueleza kwa kipindi cha miaka 19 iliyopita.Bin Laden aliuwawa na wanajeshi wa Marekani nchini Pakistan katika mji wa Abbotabad mwaka 2011.Islamad ilionekana kushirikiana na rais wa Marekani wakati huo Barack Obama katika operesheni hiyo ya kumuua Bin Laden.Inawezekana kwamba haikuwa na chaguo jingine bali kuiunga mkono Marekani.

Lakini kutokana na ukweli kwamba kiongozi huyo wa zamani wa alqaeda alikuwa akijificha katika mji huo,masuali mengi yaliibuka kuhusu uungaji mkono wa Pakistan katika harakati za magaidi.

Soma zaidi: Chuki dhidi ya Uislamu: Imran Khan ajenga daraja kati ya mashariki na magahribi

Na bila ya kusahau kwamba serikali hiyo ya Islamabad ilikuwa ikipokea mabilioni ya dola kutoka Washington kuwaandama viongozi wa alqaeda na Taliban. Hapana shaka kwa hivyo dhima ya ulaghai ya Pakistan katika vita dhidi ya ugaidi siku zote imekuwa ni tatizo kwa nchi za Magharibi ambazo zinahitaji uungaji mkono wa nchi hiyo kuudhibiti mgogoro huo lakini hazina usemi kuhusu sera ya nchi hiyo kuhusu masuala yake ya nje na ndani.

Uungwaji mkono wa itikadi kali waota mizizizi Pakistan

Ungaaji mkono wa makundi ya itikadi kali umekita mizizi ndani zaidi nchini Pakistan kuanzia ndani ya dola mpaka kwenye ngazi za kijamii. Na hakika ni chombo cha kuchochea hisia za kuipiga India na kuendelea kuwaweka majenerali wa kijeshi katika nafasi yenye nguvu.Tangu hapo uhusiano wa karibu wa waziri mkuu Imran Khan na jeshi sio siri na kwa hivyo kile alichokisema waziri mkuu huyo kuhusu Bin Laden kimsingi kinaakisi sera ya dola.

Sasa basi asilaumiwe waziri mkuu huyo kwa kusema kitu ambacho wengi walioko kwenye nafasi za mamlaka makubwa ndicho hasa wanachokiamini japo hawasemi hadharani na bila shaka hakizungumzwi hata bungeni.

Ingawa pia kwa upande mwingine waziri mkuu Khan anapaswa kuweka wazi mbele ya Marekani kwamba serikali yake haitoshirikiana katika vita dhidi ya ugaidi. Juu ya hilo Pakistan inapaswa kukoma kujiona muhanga. Khan anaendelea kuukumbusha ulimwengu kwamba Pakistan iliathirika sana kwa kushiriki katika vita dhidi ya ugaidi.

Maelfu ya raia na wanajeshi waliuwawa na makundi ya wanamgambo tangu mwaka 2001,sasa ikiwa wale waliowauwa watu wasiokuwa na hatia ni ''Mashahid'' basi waziri mkuu hana haki ya kuzungumzia juu ya kujitowa muhanga kwa nchi yake.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW