India na Pakistan zafungua tena viwanja vya ndege
12 Mei 2025
India na Pakistan zimefungua tena viwanja vya ndege ambavyo vilifungwa kufuatia kuongezeka kwa mvutano wa kijeshi kati ya mataifa hayo mawili. Hatua hii imekuja baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Marekani kuanza kutekelezwa mwishoni mwa wiki, na kuleta utulivu wa awali katika maeneo ya mpakani.
Mamlaka ya viwanja vya ndege ya India imethibitisha kuwa viwanja 32 vya ndege vilivyoko katika maeneo ya kaskazini na magharibi mwa nchi hiyo, ambavyo vilisitisha huduma kutokana na tishio la vita, sasa vimefunguliwa tena. Safari za ndege za kiraia zinaruhusiwa mara moja. Pakistan pia ilitangaza hatua kama hiyo siku ya Jumamosi.
"Hii ni hatua muhimu kwa usafiri wa raia na pia kwa utulivu wa kikanda,” alisema afisa mmoja mwandamizi kutoka mamlaka ya anga ya kiraia ya India.
Ufungwaji wa viwanja hivyo ulikuwa umeathiri vibaya ratiba za usafiri wa ndani na kikanda, hasa karibu na eneo la msitari wa udhibiti. Kwa kufunguliwa tena, maelfu ya abiria waliokwama wanatarajiwa kuendelea na safari zao kama kawaida.
Majenerali wa jeshi kujadili utekelezaji wa makubaliano
Wakati usafiri wa anga ukianza kurejea, makamanda wa kijeshi wa India na Pakistan wanapanga kukutana ili kujadili hatua zinazofuata za kuimarisha usitishaji mapigano. Mkuu wa majeshi wa India na mwenzake wa Pakistan wanatarajiwa kufanya mazungumzo moja kwa moja Jumatatu jioni.
Soma pia: India na Pakistan zaendelea kushambuliana
Waziri Mkuu wa India Narendra Modi alifanya kikao cha ngazi ya juu na mawaziri pamoja na wakuu wa majeshi mara baada ya makubaliano hayo. Jeshi la India limesema kuwa usiku wa Jumamosi ulikuwa wa kwanza kuwa na utulivu baada ya siku kadhaa za mapigano makali.
"Leo kuna pumzi ya afueni, lakini bado kuna tahadhari miongoni mwa raia,” alisema mwandishi wa DW, Shalu Yadav, akiwa umbali wa kilomita 24 kutoka Msitari wa Udhibiti.
Licha ya hali kutulia, tahadhari bado imetawala. Msemaji wa jeshi la Pakistan, Luteni Jenerali Ahmed Sharif Chaudhry, alionya kuwa mzozo mwingine wowote unaweza kuhatarisha maisha ya mamilioni.
"Hakuna nafasi ya vita kati ya New Delhi na Islamabad,” alisema. "Mtu yeyote anayejaribu kuibua vita, anatengeneza njia ya maangamizi ya pande zote.”
Amesisitiza kuwa jeshi la Pakistan lilijibu kwa "hekima” wakati wa vurugu zilizopita, akionya juu ya madhara kwa watu zaidi ya bilioni 1.6 wa ukanda huo.
Shambulio la Pahalgam labadili mchezo
Vurugu hizo zilichochewa na shambulio baya katika eneo la Pahalgam, Kashmir inayosimamiwa na India, ambalo balozi wa Ujerumani nchini India, Philipp Ackermann, alilitaja kuwa "lililobadili mchezo.” Akizungumza na gazeti la Indian Express, Ackermann alionesha mshikamano na India na kusisitiza haja ya kupunguza mvutano.
"Hili lilikuwa shambulio dhidi ya moyo wa India,” alisema. "Serikali zote mbili zinajua kuwa kupunguza mvutano ndiyo ajenda kuu kwa sasa.”
Kwa kufunguliwa kwa anga na kuanza kwa mazungumzo ya kijeshi, India na Pakistan zinaonekana kuchukua hatua za awali kuelekea utulivu — ingawa hali bado ni ya tahadhari.