1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

India na Pakistan zapimana nguvu Kashmir

1 Machi 2019

India na Pakistan wanaendelea kufyetuliana mizinga kuelekea mpaka wa Kashmir. Mtu mmoja ameuwawa huku mzozo wa mataifa hayo mawili hasimu ukizidi makali.

Infografik Karte Kaschmirkonflikt PT

Ingawa ahadi ya Pakistan ya kumuachia huru rubani wa ndege ya India imepunguza kitisho cha kuenea mzozo huo, hata hivyo mizinga haijasita bado katika eneo hilo la milima ya Himalaya lililogawika tangu mwaka 1947 kati ya  majirani hao wawili.

Mzozo huo umezidi makali wiki hii pale ndege za kivita za nchi hizo mbili hasimu zilipoingia katika eneo la adui kwa mara ya kwanza baada ya miongo kadhaa na kupelekea jumuia ya kimataifa kuhofia mzozo huo utazidi makali.

India na Pakistan kila mmoja anadai haki ya kumiliki eneo hilo la milima wanakoishi jamii kubwa ya waislam. Nchi hizo mbili zimeshateremka vitani mara mbili kwaajili hiiyo.

Wapakistan baada ya jeshi kuzidungua ndege mbili za kivita za IndiaPicha: picture-alliance/Photoshot/J. Dar

Rubani aachiwa kwasababu za kiutu

Pakistan inapanga kumuachia huru rubani wa India aliyekamatwa kufuatia mapigano ya wiki hii. Luteni kanali Abhinandan Varthaman  ataachiwa huru katika eneo la mpakani la Wagah lililoko kati ya mji wa Pakistan wa Lahore na ule wa Amristar nchini India. Maelfu ya watu wamekusanyika upande wa India kumpokea yule wanaemtaja kuwa shujaa. Akitangaza uamuzi huo waziri mkuu wa Pakistan, Imran Khan amesema hiyo ni ishara ya amani kuelekea India. Nae wakili Shiraz Anjum anashadidia kutokana na "Sababu za kiutu na kulingana na makubaliano ya Geneva, Pakistan haiwezi kuendelea kumshikilia rubani huyo wa India. Anabidi akabidhiwe serikali ya India wakati wowote ule. Sisi wapakistan tunaharakisha ili tuuonyeshe ulimwengu tunaheshimu utu."

Wanajeshi wa India na mabaki ya ndege iliyodunguliwa ya PakistanPicha: Reuters/A. Fadnavis

Upinzani nchini India unataka kujua kama opereshini imefana

Viongozi wa dunia wamekuwa wakiwahimiza viongozi wa nchi hizo mbili wajizuwie baada ya mzozo huo kuzidi makali kufuatia shambulio la bomu lililoangamiza maisha ya wanajeshi 40 wa India february 14 iliyopita.

Mzozo huu mpya unatokea wakati mgumu kwa waziri mkuu wa India Narendra Modi anaekabiliwa na uchaguzi mkuu unaobidi uitishwe mwezi may unaokuja. Upande wa upinzani unataka upatiwe maelezo kwa umbali gani opereshini ya kijeshi ya ndege za India zimefana huko Kashmir.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters

Mhariri: Yusuf Saumu

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW