1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

India yaimarisha ulinzi

28 Februari 2019

Waziri mkuu wa Pakistan Imran Khan ameahidi kumuachia huru rubani wa ndege ya kijeshi ya India, hatua inayochukuliwa kama inaweza kupunguza mzozo mkali unaotokota na India, mataifa yanayozozania eneo la Kashmir.

Indien Mirage 2000 Kampfjet in Unnao, Uttar Pradesh
Picha: Reuters/P. Kumar

Waziri mkuu Khan, ametoa tangazo hilo kwenye hotuba mbele ya mabunge ya nchi hiyo , akisema alijaribu kuwasiliana na waziri mkuu mwenzake wa India, Narendra Modi siku ya Jumanne, akimpa ujumbe kwamba anataka kutuliza hali inayofukuta baina yao.

"Kesho(Ijumaa, 01.03.2019) tutamuachia rubani wa India, kama ishara njema" Khan aliwaambia wabunge. Hakusema hata hivyo iwapo kuachiwa huko kulikuwa na masharti.

Afisa wa serikali ya India, alipozungumza kwa sharti la kutotajwa jina kwa kuwa hakuwa ameruhusiwa kuzungumza, alionya kwamba hata kama rubani huyo ataruhusiwa kurudi nyumbani, india haitasita kumshambulia jirani yake huyo kwanza, iwapo itakuwa na hofu ya mashambulizi ya wanamgambo kama yaliyotokea.

Mapema, waziri mkuu Modi alionya kwamba maadui wa India wanalenga kuvuruga hali ya utulivu nchini humo kupitia mashambulizi ya kigaidi.

Bila ya kutoa maelezo zaidi, waziri mkuu Khan, pia alisema kwamba alikuwa na hofu ya India kuanzisha mashambulizi ya makombora, usiku wa Jumatano, lakini hali ilitulizwa baadae.  

jeshi la India likionyesha ndege ya Pakistan inayodai kuitunguaPicha: Reuters/A. Fadnavis

Amesema, "Pakistan inataka amani, lakini hilo halitakiwi kuchukuliwa kama udhaifu wao" Aliongeza kuwa "ukanda utaimarika iwapo kutakuwa na amani na utulivu. Ni vizuri kwa pande zote".

Katika hatua nyingine, kumezuka mapigano mapya Alhamisi hii kati ya wanajeshi wa India na Pakistan katika eneo linaloitwa Mstari wa Udhibiti, ambalo linatenganisha eneo linalozozaniwa la Kashmir kati ya mataifa hayo mawili.

Jeshi la India limesema, wanajeshi wa Pakistan walikuwa wakilenga karibu vituo vya kijeshi vya India. Msemaji wa jeshi la India, Luteni Kanali Devender Anand, ameyaita mashambulizi hayo kuwa ni ukiukwaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano ya mwaka 2003, yaliyofikiwa na Pakistan na India.

Lakini majeshi ya la India baadae yalisema jeshi la nchi hiyo liko imara, licha ya ahadi ya Pakistan ya kumuachia huru rubani wa ndege yake wiki hii. "Tumejiandaa kikamilifu na tuko tayari kabisa kujibu uchokozi wowote kutoka Pakistan", amesema Meja Jenerali Surendra Singh Mahal kwenye mkutano na waandishi wa habari.   

Majenerali wa juu wa vikosi vya anga, ulinzi na majini nchini humo, yalidai tena kwamba India imeitungua ndege ya kivita ya Pakistan, F-16, wakati wa mashambulizi ya angani, yaliyofuatia shambulizi la Jumatano kwenye vituo vyake vya kijeshi katika eneo la Kashmir. Hata hivyo, Pakistan inakana kuwa ndege yake ilidunguliwa.

APE/AFPE

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW