1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na HakiIndia

India: Wanawake wanasiasa kutapata viti vingi Bungeni

Angela Mdungu
27 Septemba 2023

Ingawa ni suala lililochukuwa muda mrefu, lakini hatimaye India imepitisha sheria inayowahakikishia wanasiasa wanawake viti vingi zaidi, katika bunge la nchi hiyo. Hatua hiyo bado inatazamwa kama mtihani kwa taifa hilo.

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi akiwa katika moja ya mikusanyiko ya hadhara ya wanawake
Waziri Mkuu wa India Narendra Modi akiwa katika moja ya mikusanyiko ya hadhara ya wanawakePicha: AP Photo/picture alliance

India inasherehekea mafanikio makubwa kwa wanasiasa wanawake baada ya hivi karibuni, bunge la nchi hiyo, kwa sauti moja kupitisha sheria inayowahakikishia wanasiasa wa kike theluthi moja ya viti kwenye bunge la chini, pamoja na bunge la taifa lenye majimbo 28.

Kwa Waziri Mkuu Narendra Modi, sheria hiyo ni hatua muhimukwa "Naya Bahrat" yaani India mpya ambayo itajadiliwa katika vizazi vingi vijavyo.

Pamoja na mafanikio hayo, sheria hiyo itachukuwa muda ili iwe katika uhalisia.

Maafisa wanatahadharisha kwamba, kanuni mpya hazitatekelezwa kwa wakati ili zifae kutumika katika uchaguzi uliopangwa kufanyika  Mei 2024.

Soma pia:Ujerumani, Brazil, Japan na India zataka mageuzi Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Mswada huo unatarajiwa kuanza kutumika mara baada ya sensa ijayo ya India, na baada ya mchakato wa kuweka upya mipaka ya maeneo bunge utakayofanyika 2026. 

Mchakato huo pia utabadilisha idadi ya viti katika bunge na mabunge ya majimbo.

Wadau haki za wanawake hawajaridhishwa

Wanaharakati wengi na wanasiasa hawaridhishwi na sababu zilizowasilishwa za kuchelewesha kuanza kutumika kwa sheria hiyo.

Mkuu wa kituo cha utafiti wa sera cha mjini Delhi Yamini Aiyar anasema kama kweli vyama vya siasa vina nia ya dhati ya kuongeza uwakilishi wa wanawake hakuna cha kuwazuia kuhakikisha kuwa wanatoa nafasi nyingi zaidi katika uchaguzi mkuu.

Wanaharakati wa haki za wanawake IndiaPicha: Altaf Qadri/AP Photo/picture alliance

Majaribio ya awali ya kupitisha muswada  yamekuwa yakikwamishwa tangu mwaka 1996 huku wabunge wakitoa upinzani mkali.

Pamoja na ongezeko linaloridhisha la wapiga kura wanawake katika chaguzi za hivi karibuni, wanawake wanaotaka kujiingiza katika siasa bado wanakabiliwa na vikwazo vya kimfumo vilivyoota mizizi  India.

Soma pia:India yamfukuza balozi wa Canada

Changamoto hizi zinaweza kuhusishwa na mitazamo ya kijamii, ubaguzi na ukosefu wa upatikanaji wa rasilimali.

Kulingana na shirika la Umoja wa mabunge duniani, IPU  kinachokusanya taarifa kuhusu mabunge ya kitaifa ulimwenguni, India ni ya 141 kati ya nchi 187 katika suala zima la uwakilishi wa wanawake bungeni.

Shirika hilo ambalo limekuwa likifuatilia na kuwawezesha wabunge wa kike kwa miongo mingi limesema kuwa kwa ujumla, mazingira katika vyama vya siasa hayakuwa rafiki kwa wanawake.

Hali ya usawa wa kisiasa India hairidhishi

India ilipata Waziri wake Mkuu mwanamke Indira Gandhi, kwa mara ya kwanza mwaka 1966.

Wanawake, pia wamekuwa wakichaguliwa kuwa mawaziri wakuu wa majimbo na 11 kati ya hao sasa ni mawaziri kwenye serikali ya Waziri Mkuu Modi.

Hata hivyo data za sasa zinathibitisha kuwa, uwakilishi wa wanawake bado hautoshi.

Bunge la India likiwa katika vikao vyake Picha: AP Photo/picture alliance

Katika bunge la chini  la Lok Sabha lililo chini ya bunge la taifa, wabunge wanawake ni asilimia 15 pekee, yaani kuna wabunge wanawake 83 kati ya 543.

Katika baraza la majimbo, wawakilishi wanawake ni asilimia 13 pekee.

Soma pia:India yaweka vizuizi baada ya wawili kufa kwa virusi- Nipah

Hadi sasa, hakuna jimbo la India lenye zaidi ya asilimia 18 ya wawakilishi wanawake bungeni.

Majimbo ya Himachal Pradesh na Mozoram  kwa mfano yana mwanamke mmoja kila moja.

Zaidi ya hapo, majimbo saba hayakupeleka mbunge hata mmoja mwanamke bungeni katika uchaguzi wa mwaka 2019.

Sheria mpya ya hivi karibuni, inatarajiwa kusaidia kupunguza pengo la kijinsia mara tu itakapoanza kutekelezwa.

Lakini hata kabla ya hapo, vyama vya siasa vya India vinaweza vikaamua kuwaruhuhusu wagombea wanawake wengi zaidi wagombee katika uchaguzi ujao wa mwaka 2024.
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW