1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ines Pohl: Matokeo ya uchaguzi wa Thuringia ni aibu

6 Februari 2020

Waziri Mkuu amechaguliwa kwa kuungwa mkono na chama cha siasa kali za mrengo wa kulia AfD. Kukiukwa kwa maadili kunaonyesha wazi jinsi upinzani dhidi ya kuongezeka kwa ushawishi wa mrengo wa kulia Ujerumani ulivyo.

Braunschweig AfD-Bundesparteitag Höcke
Picha: DW/K.-A. Scholz

Huu hapa uchambuzi wa mhariri mkuu wa DW Ines Pohl.

Wiki moja iliyopita mnamo Januari 29 2020 bunge la Ujerumani, Bundestag, lilifanya maadhimisho ya walioangamia katika mauaji ya halaiki ya Holocaust. Hafla hiyo ilikuwa ni maadhimisho ya 75 ya uhuru wa kambi ya mauaji ya Auschwitz.

Alipokuwa akilihutubia bunge hilo, Rais wa Israel Reuven Rivlin aliwataka Wajerumani wasisahau yaliyopita akiwataka wasimame kidete katika suala la chuki dhidi ya Wayahudi, ubaguzi wa rangi. Rivlin alisema Wajerumani na vyama vyao vya kisiasa wana jukumu maalum kwa wale wanaofurahia kuwa na uhuru na maadili ya demokrasia.

Na sasa wiki moja tu haya yametokea, mwanachama wa chama cha Free Democratic Party FDP amechaguliwa kuwa waziri mkuu wa jimbo la mashariki mwa Ujerumani la Thuringia kwa usaidizi wa chama cha mrengo wa kulia cha Alternative für Deutschland AfD.

Picha: DW/M. M. Rahman

Ni kura iliyoishtua Ujerumani

Ni kura iliyoishtua Ujerumani. Kura inayoonyesha wazi kuwa wanasiasa kutoka chama chake Kansela Angela Merkel cha CDU na kile cha FDP, vyama ambavyo vyote viliiunga mkono kura hiyo, hawalielewi jukumu lao la kihistoria. Ni kura ambayo kwa sasa inatoa mtihani kwa vyama vya kidemokrasia vya Ujerumani, mtihani ambao huenda ukapelekea kuandaliwa kwa uchaguzi mpya wa shirikisho.

Wiki chache zijazo zitaonyesha iwapo zile ahadi zilizotolewa na wanasiasa mashuhuri wa Ujerumani kwamba hawatounda muungano na chama cha AfD zina maana yoyote au ulafi wa madaraka una nguvu kushinda ahadi zao.

Ingawa mwenyekiti wa chama cha CDU Annegret Kramp-Karrenbauer amewakataza wanachama wa CDU katika jimbo la Thuringia kuingia katika muungano na AfD, wanaweza kujiunga na chama hicho. Kwa hiyo kutokuwa kwake na udhibiti kunamaanisha nini?

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel atafanya nini iwapo wanachama wa CDU katika jimbo hilo watajiunga kweli na AfD na kiongozi wake Björn Höcke? Höcke alisema Wajerumani ni wenda wazimu kwa kuweka mnara wa aibu kwa ajili ya Wayahudi waliouwawa. Na chama cha Social Democratic SPD kitafanya nini? Je, kitajiondoa kutoka kwenye serikali ya muungano ambayo ni mshirika na kupelekea kufanyika kwa uchaguzi mpya?

Siku hii imeitikisa Ujerumani mno, kilichosalia sasa ni vyama vya kidemokrasia Ujerumani kuonyesha mshikamano wao. Na ni kipi ambacho wako tayari kukifanya katika juhudi za kuhakikisha kwamba uchaguzi huu unasahaulika?

Uchaguzi huu unaonyesha wazi jinsi Wajerumani walivyoisahau historia yao na jinsi onyo la rais Rivlin kwamba Ujerumani haistahili kuanguka tena, ni onyo la kila Mjerumani. Ni jambo linaloonyesha pia kwamba nchini Ujerumani, hakuna anayestahili kujidanganya kwamba historia haiwezi kujirudia.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW