1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Kandanda

Infantino ataka Urusi irejeshwe mashindano ya kimataifa

5 Februari 2026

Rais wa Shirikisho la soka duniani FIFA, Gianni Infantino, amesema anaunga mkono Urusi kurejeshwa kwenye mashindano ya kimataifa ya mpira wa miguu.

Urusi | Putin - Infantino 2019
Rais wa Urusi Vladimir Putin akisalimiana na Rais wa FIFA Gianni Infantino 2019Picha: Yuri Kadobnov/AFP via Getty Images

Rais wa Shirikisho la soka duniani FIFA, Gianni Infantino, amesema anaunga mkono Urusi kurejeshwa kwenye mashindano ya kimataifa ya mpira wa miguu na anataka kumaliza adhabu ya miaka minne ambayo nchi hiyo imewekewa tangu ilipoanza kuivamia Ukraine mnamo Februari 2022.

FIFA iliipiga Urusi marufuku, ikiindoa kwenye Kombe la Dunia la 2022 na kuwaondoa kwenye hatua za kufuzu Kombe la Dunia la 2026.

Akizungumza na kituo cha Sky Sports, Infantino amesema kwamba marufuku hiyo "haijazaa matunda” na badala yake imeongeza hasira na mgawanyiko.

Anapendekeza angalau timu za vijana za Urusi ziruhusiwe kurejea kwenye mashindano ya Ulaya. Hata hivyo, Shrikisho la mpira wa miguu barani Ulaya UEFA linaloweza kufanya uamuzi huo limesema kuwa vita lazima vikome kabla ya Urusi kuondolewa marufuku hiyo.

Mwaka 2023, UEFA ilijaribu kuruhusu timu za chini ya miaka 17 kutoka Urusi, lakini ilifuta uamuzi wake baada ya mashirikisho 12 kutishia kususia mechi.

Kwa sasa, Urusi inacheza mechi za kirafiki tu, ikiwemo dhidi ya Chile na Peru ilizocheza mnamo Novemba 2025.

Infantino anapinga marufuku za kisiasa kwenye michezo na anataka FIFA "iweke kwenye katiba" kwamba mataifa hayapaswi kufungiwa kutokana na vitendo vya viongozi wao wa kisiasa.

Kamati tendaji ya UEFA ambayo itakutana tena tarehe 11 Februari huko Brussels, ndiyo yenye mamlaka ya kuamua kama Urusi inaweza kurejeshwa kwenye mashindano ya Ulaya. Urusi ilikuwa mwenyeji na kufikia hadi robo fainali ya Kombe la Dunia la mwaka 2018 wakati wa muhula wa kwanza wa Infantino kama rais wa FIFA.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW