Inter Miami yamkaribisha rasmi Messi
17 Julai 2023Tuelekee Marekani ambapo kama wewe ni Lionel Messi hakuna kinachoweza kuwazuia mashabiki wako kujitokeza kukutizama. Na hata mvua kubwa haikuweza kuharibu karamu ya kumkaribisha Lionel Messi katika klabu ya Inter Miami jana Jumapili huko Fort Lauderdale, Florida, ambapo sura mpya ya Ligi Kuu ya Soka (MLS) ilitambulishwa kwenye uwanja uliojaa mashabiki
Messi mshindi mara saba wa tuzo ya mchezaji bora duniani ya Ballon d'Or alitambulishwa kwa mashabiki katika hafla hiyo ya kufana katika dimba la nyumbani la klabu ya Miami
"Kwanza kabisa, napenda kuwashukuru watu wote wa Miami kwa makaribisho na upendo wao tangu nilipowasili katika jiji hili. Ukweli ni kwamba nina furaha sana kuwa hapa Miami na kuwa nanyi. Niko tayari kuanza mazoezi na kushuka dimbani. Niko hapa na hamu ambayo nimekuwa nayo kila wakati ya kushindana, ya kutaka kushinda, na kusaidia klabu kuendelea kukua."
Messi mwenye umri wa miaka 36 alisaini mkataba na Inter Miami ambao utamuweka klabuni hapo hadi 2025. Nyota huyo huenda akapigilia uzi wake mpya katika mechi ya Ijumaa ya Kombe la Ligi dhidi ya Cruz Azul ya Mexico.
Kuwasili kwa Messi ni chachu kubwa kwa sifa ya kandanda la Marekani, ambayo itaandaa Kombe la Dunia la 2026 kwa Pamoja na Mexico na Canada
ap