1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Intermilan wapeperusha bendera ya Serie A

10 Februari 2020

Mabingwa mara nane mfululizo wa ligi ya Serie A Italia, Juventus, wameondolewa katika uongozi wa ligi hiyo na Intermilan. Inter wamefanikiwa baada ya kutoka nyuma mabao mawili walipokuwa wakicheza na AC Milan Jumapili.

Italien Seria A Inter Mailand Romelu Lukaku
Picha: picture-alliance/AP Photo/L. Bruno

Mechi hiyo ilikuwa ni dabi ya jiji la Milan na Intermilan wakaonyesha ubabe wao kwa kutoa ushindi wa magoli mane kwa mawili.

Ante Rebic ndiye aliyewaweka AC Milan kifua mbele mnamo kipindi cha kwanza baada ya kuandaliwa pasi na Zlatan Ibrahimovic kisha Ibrahimovic mwenyewe akaongeza bao la pili katika kipindi hicho hicho cha kwanza na kuwapelekea Milan kumaliza kipindi cha kwanza wakiwa wanaongoza kwa mabao mawili.

Ila kipindi cha pili kocha Antonio Conte wa Inter alikuwa na mawazo mengine kwani mchezaji wa Manchester United aliye kwa mkopo hapo Inter Alexis Sanchez alisaidia kuunda mabao mawili baada ya Brozovic kucheka na wavu na kufunga goli la kwanza.

Kocha wa zamani wa Chelsea Antonio Conte anaifunza Inter sasaPicha: picture-alliance/dpa/I. Langsdon

Mabadiliko yaliyofanywa na Conte mnamo kipindi cha pili yalileta matunda kwani Victor Moses alimuandalia Romelu Lukaku krosi nzuri aliyoifunga kwa kichwa na kuwapelekea Intermilan kuebuka kidedea nne kwa mbili.

Kabla mechi hiyo, Juventus walikuwa wamechapwa mabao mawili kwa moja na Hellas Verona licha ya Cristiano Ronaldo kufunga katika mpambano huo.

Sasa Intermilan wako sawa kialama na Juventus kileleni mwa ligi hiyo kila mmoja akiwa na pointi hamsini na nne ila Inter wamewazidi Juventus kwa wingi wa magoli na ndio sababu wanaongoza. Lazio hawako mbali kwani wana alama hamsini na tatu katika nafasi ya tatu.