Intifadha imerudi, wasema wahariri
19 Novemba 2014Mhariri wa Thüringische Landeszeitung anasema ni wazi kuwa sasa mapambano ya mitaani ya Wapalestina yamerudi kikwelikweli kwenye eneo hilo la Mashariki ya Kati na kwa kuwa maridhiano na hoja ni misamiati ya kigeni panapohusika mzozo usiotatuka na kwa Mashariki ya Kati, kuna safari refu sana kufikiwa hilo.
Kwa hivyo, anahoji mhariri huyo, kuishi pamoja baina ya Wapalestina na Waisraili ni utabiri wa kinabii tu, ambao hadi sasa haujakuwa ukweli. Kuotezana vidole vya lawama hakumsaidii yeyote. Kila upande unabeba dhima kwenye kuzorota kwa hali.
Upande mmoja unachimba mahandaki yanayoibukia kwenye upande wa pili kwa ajili ya kufanya mashambulizi. Upande mwengine unajenga makaazi ya walowezi kwenye ardhi isiyo halali na kuutafsiri msemo wa Kibiblia: "Jicho kwa jicho, jino kwa jino" kwa ukali wa hali ya juu zaidi. Na hapo, anasema mhariri huyo, kinachobakia ni intifadha.
Merkel amwalike Putin kama mshirika
Chama cha upinzani cha Die Linke sasa kinamtaka Kansela Angela Merkel kutumia kile knachokiita "siasa za kuukwamua mkwamo kati ya Urusi na Ulaya. Lakini kwa kutumia njia gani?
Gazeti la Rheinische Post linanukuu pendekezo la mkuu wa Die Linke, Katja Kipping, kwamba katika mkutano ujao wa kilele wa mataifa ya G8 ambayo Merkel atakuwa mwenyeji, kiongozi huyo wa Ujerumani anatakiwa amualike Rais Vladimir Putin wa Urusi kama mshirika sawa.
Sababu, kwa maoni ya mhariri, inaonekana Ulaya inashindwa kuichukulia Urusi kama ni mshirika bali adui na mshindani. Lakini hayo siyo maoni ya Norbert Röttgen, mwenyekiti wa kamati ya mambo ya nje bungeni kutokea chama cha CDU, ambaye anaamini kuwa lazima Ujerumani imzuie Putin hapo hapo alipokwishafika, na kisha imrejeshe nyuma, linapohusika suala la Ukraine. "Putin anaujaribu mpaka tuliomuekea, kwa kiasi gani anaweza kuuchupa, kisha atauchupa." Anasema Röttgen wa CDU.
Data za mawasiliano ziwekwe zaidi
Mhariri wa Neue Osnabrücker Zeitung anaendelea kulilia vitendo vya udhalilishaji watoto wadogo nchini Ujerumani, hasa kwenye suala zima la hifadhi ya data za mawasiliano.
Kufunguliwa kwa kesi dhidi ya mwanasiasa wa zamani wa chama cha SPD, Sebastian Edathy, kumelifanya Shirika la Ujasusi la Ujerumani (BDK) kutoa wito wa kuwepo sheria maalum kwa ajili ya muda ambao data za mawasiliano zinaweza kuhifadhiwa.
Mkuu wa BDK, Andre Schulz, anasema kesi ya Edathy inaonesha kuwa ni muhimu na kuna manufaa makubwa kuhifadhi data za mawasiliano ya simu kwa muda mrefu, maana lau kama isingelikuwa hivyo, kesi inayomuhusu mwanasiasa huyo ya kukutwa na picha za watoto wadogo wakiwa utupu, ingelikwishakufa.
Ikiwa wito huu wa mkuu wa ujasusi wa Ujerumani utasikilizwa, basi sasa data za mawasiliano zinaweza kuhifadhiwa kwa zaidi ya miezi mitatu, na pengine watoto wengi zaidi wakaokolewa na unyanyasaji wa mitandaoni, anahitimisha mhariri huyo.
Mwandishi: Mohammed Khelef
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman
Vyanzo: Thüringische Landeszeitung, Neue Osnabrücker Zeitung, Rheinische Post