IOC yakutana na wadau wa michezo kujadili athari za Corona
17 Machi 2020
Wasiwasi kuhusiana na endapo michezo ya Olimpiki iliyotarajiwa kuanza Julai 24 hadi Agosti 9 umezidi kuongezeka siku baada ya siku hasa kutokana na uwepo wa virusi hatari vya Corona, ambavyo hadi hivi sasa vimewaathiri takribani watu 180,000 na kuuwa zaidi ya watu 7,000 duniani ambapo kwa sasa bara la Asia ndilo limekuwa chimbuko la virusi hivyo.
Mashindano ya michezo yamesimama kwa muda barani Ulaya, na hivyo kuzuia mandalizi ya wanariadha kwa ajili ya michezo ya Olimpiki ya Tokyo.
Hakuna maamuzi yanayotarajiwa kutoka kwa kamati ya IOC wiki hii, huku mabilioni ya fedha yakiwa tayari yamekwishawekezwa katika miuondombinu ya michezo pamoja na viwanja nchini Japani, IOC na ulimwengu pamoja na wadhamini wa ndani na wamiliki wa haki za matangazo.
IOC pamoja na wandaaji wa michezo hiyo ya Olimpiki nchini Japani bado wana imani kwamba michezo hiyo itafanyika kama ilivyokuwa imepangwa, lakini virusi vya Corona vimevuruga michezo ya kutafuta tiketi ya kufuzu katika mashindano hayo.
"Kunatarajiwa kuwa muendelezo wa mikutano itakayoendeshwa kwa njia ya simu katika siku za usoni kwa ajili ya kujadili masuala hayo," chanzo kutoka ndani ya kamati ya IOC kimeliambia Shirika la habari la Reuters katika mazungumzo yake.
IOC itaendelea kuyafahamisha mashirikisho na kamati ya kitaifa ya Olimpiki, NOC, kuhusiana na hali hiyo na kujadili kwa pamoja kuhusiana na michezo na mchakato wa kufuzu."
Jumatatu (16.03.2020) Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki, IOC, iliondoa mashindano yote ya ndondi kuwania tiketi ya kufuzu kushiriki michezo ya Olimpiki huko Tokyo, Japan mwaka huu 2020 kwa ajili ya kukinga afya za wanariadha na waangalizi wa michezo hiyo lakini yaelezwa kuwa kutakuwepo na baadhi ya matukio ya kufuzu tiketi ya kushiriki michezo hiyo ya Tokyo mwaka huu wa 2020. Kamati hiyo imesisitiza kwamba bado inashikilia msimamo kuwa michezo hiyo ya Tokyo 2020 itafanikiwa.
Maelfu ya washiriki wa Olimpiki kwa sasa hawawezi kusafiri, kufanya au kujishughulisha na mazoezi hasa kutokana na vikwazo vilivyowekwa na nchi mbalimbali huku kukiibuka maswali kuhusiana na ubora na viwango vya mashindano ya Tokyo ni lazima michezo hiyo iendelee.
Jumanne (17.03.2020) Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe alisema kuwa kundi la viongozi saba limekubaliana kuunga mkono kukamilisha mashindano ya Olimpiki lakini wakiepuka maswali kuhusu huenda viongozi wengine wamesababisha uwezekano wa kuahirishwa kwa michezo hiyo.
Katika mkutano usio wa kawaida wa viongozi wa G7 kwa njia ya vidio kujadili janga la virusi vya Corona, Waziri mkuu Abe alisema kuwa aliwaambia: "Tunafanya kila kitu katika mamlaka yetu kuandaa michezo hiyo kikamilifu ili kuthibitisha kuwa binadamu ana uwezo wa kulishinda janga la Corona."
Chanzo: Reuters.