1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IPC yasema mji wa El-Fasher Sudan wakabiliwa na njaa

4 Novemba 2025

Kundi la uangalizi wa njaa duniani IPC limesema kuwa maeneo mawili ya Sudan yanakabiliwa na njaa ambayo iko kwenye hatari ya kuenea katika maeneo mengine ya nchi hiyo.

Sudan El Fasher 2025 | Ein Mädchen bereitet in einem Flüchtlingslager in der Region Nord-Darfur Essen zu
Picha: UNICEF/Xinhua/picture alliance

IPC inasema kuna njaa katika eneo la El-Fasher huko magharibi mwa Darfur na katika mji wa Kadugli ulioko katika mkoa wa South Kordofan.

Hayo yakiarifiwa watu saba wameuwawa katika shambulizi la droni lililofanywa katika hospitali ya watoto nchini Sudan.

Haya ni kwa mujibu wa madaktari katika taifa hilo lililozongwa na mapigano. Wanawake na watoto ni miongoni mwa waliouwawa kwenye shambulizi hilo lililofanywa eneo la Kernoi karibu kilomita 270 kutoka mji wa El-Fasher katika eneo la Darfur.

Wakati huo huo, mahakama ya Kimataifa ya Jinai, ICC, imeonya kuwa ukatili unaofanywa huko El-Fasher, unaweza kuwa uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita.

ICC imeyasema haya baada ya Umoja wa Mataifa kudai kuwa maelfu ya watu wamelikimbia eneo jirani na El-Fasher ambalo limetekwa na wanamgambo wa RSF kwa sasa.