1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ipi hatma ya kesi zinazomkabili Donald Trump?

15 Novemba 2024

Donald Trump anatarajiwa kuapishwa mnamo mwezi Januari kuingia tena Ikulu lakini bado anakabiliwa na kesi kwenye majimbo na pia kitaifa. Je, nini kitatokea?

West Palm Beach Florida | Wahlsieger Trump bei Wahlparty
Picha: Alex Brandon/AP/picture alliance

Hadi siku ya uchaguzi wa rais wa Marekani tarehe 5 Novemba, Donald Trump, alikuwamo katika hatari ya kwenda jela.  Lakini kurejea kwake Ikulu mwaka ujao kunamaanisha kuwepo uwezekano wa kesi kadhaa zilizo mahakamani kutenguliwa ikiwa pamoja na hukumu iliyotolewa na mahakama ya mjini New York inayohusu kughushi nyaraka za biashara.

Mabadiliko katika kesi zinazomkabili Trump yanatokana na uamuzi wa Mahakama ya Juu kwamba marais wana kinga kubwa ya kutoshtakiwa kwa vitendo wanavyofanya wanapokuwa madarakani.

Hukumu hiyo iliwalazimu waendesha mashtaka katika kesi mbili kuangalia upya ili kubainisha iwapo wangeliweza kufanikiwa. Wakati wa muhula wake wa kwanza Trump aliwateua majaji watatu kwenye Mahakama ya Juu na hivyo kuongeza idadi ya majaji wahafidhina kufikia sita.

Na kwa sababu, sera ya wizara ya sheria inasema rais aliyemo madarakani hawezi kufunguliwa mashtaka kwenye Mahakama ya Juu, mwendesha mashtaka sasa anafunga virago vya uchunguzi.

Kesi zipi zinamkabili Trump na mwelekeo wake utakuaje? 

Trump kwenye mahakama ya mji wa New York kusikiliza moja ya kesi zake.Picha: Steven Hirsch/Pool/REUTERS

Trump anakabiliwa na mashtaka manne ya jinai: mawili katika ngazi ya kitaifa, moja kwenye jimbo la New York na lingine katika jimbo la Georgia.

Hukumu ilitolewa kwenye mahakama ya New York pekee. Mahakama hiyo ilimtia Trump hatiani kwa makosa 34 ya uhalifu kuhusiana na njama za kushawishi uchaguzi wa mwaka 2016 kupitia malipo ya fedha ili kumnyamazisha mcheza sinema Stormy Daniels.

Hata hivyo kesi hiyo imesimamishwa hadi mwezi Novemba ili kuwapa mawakili wa pande zote muda wa kutafakari hatua zinazofuata baada ya kufanyika uchaguzi.

Trump pia anakabiliwa na kesi nyingine kadhaa za jinai. Hata hivyo watalamu wa sheria wanasema katika kipindi cha miaka minne ijayo kesi hizo huenda zikasimamishwa. Hayo  amesema Profesa wa chuo kikuu cha sheria cha Chicago, Eric Posner.

Kulingana na sera ya wizara ya sheria, rais aliyemo madarakani hafunguliwi mashtaka. Hata hivyo huenda sera hiyo isitumike kwa rais anayeingia madarakani lakini ambaye tayari ameshahukumiwa. Hata hivyo wataalamu hawaoni iwapo itawezekana kuendelea kumhukumu Trump.

Trump anaweza kuhukumiwa kwenda jela akikaribia kuchukua Urais?

Mara zote kesi za Donald Trump zimevutia wafuasi na wakosoaji wake. Picha: Angela Weiss/AFP/Getty Images

Katika kesi moja ya mahakama ya juu Trump alishtakiwa kwa makosa 34 yaliyohusu kuvunja sheria na kushiriki katika njama za kuzuia mkondo wa sheria, kesi hiyo ilitupiliwa mbali na jaji aliyemteua.

Hukumu iliyotolewa katika kesi iliyohusu fedha ambazo Trump alizolipa ili kumnyamazisha mcheza sinema Stormy Daniels bado ingalipo.

Anaweza kwenda jela lakini hakuna uhakika iwapo atasomewa hukumju hiyo mahakamani baada ya kuchaguliwa tena kuwa rais. Na endapo adhabu itatolewa inaweza kuwa faini au kifungo cha nje.

Donald Trump na wafuasi wake 18 walishtakiwa kwenye mahakama ya Georgia kwa kosa la kujaribu kuyabadilisha matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2020.

Lakini kesi hiyo imekumbwa na utata wa kisheria na upande wa mashtaka umewekwa kando, kutokana na mbinu za kujaribu kumwengua mwanasheria mkuu wa jimbo kwa madai kwamba alikuwa na uhusiano wa mashaka na mwendesha mashtaka ambaye alimteua.

Atakapomaliza muhula wake wa sasa Donald Trump atakuwa na umri wa miaka 82.  Na kwa hivyo inawezekana kwamba hakuna atakayetaka kuzifufua kesi zinazomkabili.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW