1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIran

Iran haina mpango wa kufanya mazungumzo na Marekani

28 Septemba 2026

Mvutano kati ya Marekani na Iran unaendelea kufukuta huku pande zote mbili zikizungumzia uwezekano wa mazungumzo na wa kurejea kwa mashambulizi.

Iran Tehran 2026 | Waziri wa Mambo ya Nje Abbas Araghchi na Jenerali Mohsen Rezaie katika hafla
Iran inasema iliwasilisha masharti saba ya kumaliza vita na kufungua tena Mlango-Bahariu wa HormuzPicha: Morteza Nikoubazl/NurPhoto/picture alliance

Vyombo vya habari vya serikali nchini Iran vimeripoti Jumatatu (28.09.2026) kwamba ujumbe wa Iran katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa mjini New York hauna mpango wa kufanya mazungumzo yoyote na Marekani. Hayo yanajiri baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kusema anatarajia mazungumzo zaidi kati ya pande hizo mbili.

Shirika rasmi la habari la IRNA limemnukuu chanzo kilicho karibu na ujumbe huo kikisema kuwa Iran tayari imewasilisha msimamo wake kwa Marekani kupitia mpatanishi kutoka Qatar. Kwa mujibu wa IRNA, ujumbe wa Iran unatarajiwa kurejea Tehran Jumanne.

Mlango Bahari wa Hormuz umebaki kuwa kitovu cha mvutano kati ya Marekani na Iran. Tehran inasema iliwasilisha pendekezo kupitia wapatanishi wa Qatar la kufungua tena njia hiyo ya meli ndani ya siku saba, iwapo Marekani nayo ingechukua hatua ilizoomba Iran.

Iran yaonesha uwezo wake wa makombora Tehran

01:21

This browser does not support the video element.

Rais Donald Trump amesema pendekezo hilo halikubaliki kwake. Hata hivyo, amesema anatarajia mazungumzo na Iran kuendelea wiki hii. Pia hajaondoa uwezekano wa Marekani kuanzisha tena mashambulizi ya kijeshi dhidi ya nchi hiyo.

Kwa upande wa Iran, Waziri wa Mambo ya Nje Abbas Araghchi amesema nchi yake iko tayari kwa mazungumzo, lakini pia imejiandaa kukabiliana na mashambulizi mapya.

"Tumejiandaa kikamilifu iwapo vita vitaanza tena. Tutasimama imara dhidi ya mashambulizi yoyote mapya, hata kama vita hivyo vitakuwa vikubwa sana. Lakini wakati huohuo, tuko tayari kwa diplomasia. Ni juu ya Rais Trump kuchagua", alionya Araghchi.

Araghchi anasema masharti ya Iran ni pamoja na kuachiliwa kwa mali zake zilizozuiwa na kuruhusiwa kuuza mafuta. Anadai Marekani ilikuwa imekubali hatua hizo hapo awali. Pia amesema, licha ya kauli ya Trump hadharani, Iran haikuwa imepokea taarifa rasmi kupitia wapatanishi kwamba pendekezo lake limekataliwa.

Rais Donald Trump aliliambia shirika la habari la Axios kuwa anatarajia mazungumzo kuanza tena hivi karibuni, siku moja baada ya kukataa pendekezo la Tehran la kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz ndani ya siku sabaPicha: REUTERS

Mazungumzo kati ya Saudi Arabia na Marekani

Mvutano huo unajiri wakati hali ya usalama katika eneo hilo inaendelea kuzorota. Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Mwanamfalme Faisal bin Farhan, amewasili Washington kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio. Moja ya masuala yanayotawala mazungumzo ya kikanda ni mapigano yanayoongezeka kati ya Saudi Arabia na waasi wa Kihouthi nchini Yemen.

Kwa mujibu wa vyanzo vilivyozungumza na shirika la habari la Reuters, mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia Mwanamfalme Mohammed bin Salman aliomba msaada wa kijeshi wa Marekani dhidi ya Wahouthi. Washington ilikataa kufanya mashambulizi yenyewe, lakini ilikubali kutoa taarifa za kijasusi na msaada wa kubaini maeneo ya kushambulia.

Israel yawafukuza wanadiplomasia wa Uholanzi

Katika mvutano mwingine wa kidiplomasia, Israel imefuta hadhi ya wanadiplomasia wa Uholanzi wanaowakilisha nchi yao kwa Mamlaka ya Palestina mjini Ramallah, na imewapa siku saba kuwasilisha nyaraka zao za kidiplomasia zilizotolewa na Israel.

Hatua hiyo ni jibu la Israel kwa uamuzi wa Uholanzi kusitisha uingizaji wa bidhaa kutoka kwenye makaazi ya walowezi wa Israel katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uholanzi, Tom Berendsen, ameuita uamuzi wa Israel kuwa usio wa lazima. Anasema marufuku ya bidhaa hizo inalenga kutimiza wajibu wa nchi yake chini ya sheria za kimataifa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW