Iran iko tayari kwa mazungumo ikiwa Marekani itaomba radhi
24 Juni 2020Uhasama kati ya Marekani na Iran, umeongezeka tangu mwaka 2018 wakati rais wa Marekani Donald Trump, alipoiondoa nchi yake katika mkataba wa nyuklia uliosainiwa na baina ya Iran na mataifa makubwa yaliyo na nguvu duniani mwaka 2015, na baadae kuiwekea Jamhuri hiyo ya kiislamu vikwazo vilivyouathiri uchumi wake.
"Hatuna tatizo lolote la kuwa na mazungmzo na Marekani, lakini hilo litafanyika iwapo Marekani itatekeleza wajibu wake juu ya mkataba wa nyuklia, iombe msamaha na itulipe fidia kwa kujitoa katika mkataba huo wa mwaka 2015. Lakini tunajua hii miito ya kutaka mazungumzo na Iran inayotolewa na Mmarekani ni ya uwongo mtupu," alisema Rouhani katika hotuba iliyopeperushwa moja kwa moja kupitia televisheni ya kitaifa.
Juhudi za kukaa mezani
Iran imekataa kuwa na mazungumyo ya aina yoyote na Marekani ambayo inajaribu kuishinikiza kuwa na mpango mpya, hadi pale itakapoiondolea vikwazo na kurejesha mezani makubaliano yaliyoidhinishwa awali.
Katika ujumbe aliouandika katika mtandao wake wa Twitter mapema mwezi huu, rais Trump alirejelea msimamo wake wa kutaka mpango mpya na Iran, unaonuiwa kudhibiti shughuli za kinyuklia, kusitisha mpango wake wa makombora ya masafa marefu na kumaliza vita vyake vya chini kwa chini na Marekani vilivyodumu kwa miongo kadhaa.
Katika kujibu sera ya Marekani ya kushinikiza kupata inachokitaka, Iran inaendelea kukiuka makubaliano yaliyoko katika mkataba wa nyuklia juu ya kupunguza shughuli zake za nyuklia, lakini imesema inaweza kuanza kutii tena makubaliano hayo iwapo washirika wengine wa Ulaya katika mkataba huo, watatekeleza ahadi yao ya kuilinda Iran kutokana na adhabu ya kiuchumi iliyowekewa na Marekani.
Rouhani amesema Ulaya imeshindwa kufanya kile ilichokiahidi. Rais huyo wa Iran pia alilikosoa azimio la shirika la Umoja wa Mataifa la kudhibiti matumizi ya Atomiki lililopitishwa siku ya Ijumaa, lililoitaka Iran kuacha kulinyima shirika hilo nafasi ya kuingia katika vinu viwili vya zamani vya nyuklia na kushirikiana nao kikamilifu.
Kwa kulijibu hilo Rouhani amesema taifa lake liko tayari kabisa kushirikiana na IAEA chini ya sheria.
Amesema shirika hilo yumkini likakosa uhalali wake kwa kufanya uamuzi kulingana na madai yanayotolewa na Israel ambayo ni adui mkubwa wa Iran, ambayo Rouhani amesema hayana mashiko. Israel na Marekani zinataka shirika hilo lichunguze mambo yaliyotokea miaka 20 au 18 iliyopita na kudai kuwa Iran inalidanganya shirika hilo na kulipotezea dira. Rouhani amesema shirika hilo linapaswa kufanya maamuzi yake lenyewe bila ya kushinikizwa.